Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mazishi ya aliyekuwa Askofu wa Pili wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma na Katibu Mkuu Mstaafu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Marehemu Askofu Stanford Shauri.
Mazishi hayo yamefanyika katika Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma, Liuli Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais amesema Serikali inatambua mchango mkubwa aliyoutoa Askofu Shauri katika hapa nchini, akiwa ametumikia Serikali za Mitaa kwa zaidi ya miaka 12 pamoja na kuwa katibu mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa zaidi ya miaka 10.
Aidha, Makamu wa Rais amesema Marehemu Askofu Shauri amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii pamoja na kuendeleza na kuikuza imani ya kikristo nchini.
Amesema ni dhamira ya Serikali kuendeleza yale ambayo Marehemu Askofu Shauri aliyasimamia ikiwemo masuala ya amani na haki.
Makamu wa Rais amewasilisha salamu za pole kwa familia ya marehemu, Kanisa la Anglikana, wakazi wa Ruvuma, Nyasa na wote walioguswa na msiba huo.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano mzuri iliyonayo na Taasisi za Dini katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi. Ameipongeza Serikali kwa ukarabati wa barabara kutoka Mbambabay hadi Liuli katika Wilaya ya Nyasa ambayo ilikuwa ni changamoto kubwa hali inayodhihirisha kuwajali wananchi wa eneo hilo.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
06 Mei 2026
Nyasa – Ruvuma.









0 Comments