Header Ads Widget

WAKIMBIZI WALIOTOROKA KAMBINI KUSAKWA KILA MAHALI

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma 

SERIKALI mkoani Kigoma imetangaza kuendesha operesheni maalum kuwasaka wahamiaji haramu wakiwemo  wakimbizi wa Burundi wanaotuhumiwa kukimbia kambini na kuishi mtaani bila kufuata taratibu za kisheria za masuala ya uhamiaji.


Mkuu wa mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro alisema hayo katika mkutano na waandishi ambapo alisema kuwa ipo taarifa ya  mkoa Kigoma kukabiliwa na Wimbi kubwa la raia wa kigeni kuishi bila kufuata taratibu ambapo Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye makambi mkoani Kigoma wanadaiwa kuwa chanzo cha tatizo hilo.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa Mkuu huyo wa mkoa Kigoma alisema kuwa operesheni hiyo itafanyika kila mahali ambapo wanahisi kuna dalili ya uhalifu, wahalifu na wahamiaji haramu.

Idara ya Wakimbizi ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi mwishoni mwa mwaka kupitia Mkurugenzi idara ya Wakimbizi, Sudi Mwakibasi  ilitangaza kufungwa kwa kambi ya Wakimbizi wa Burundi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma kufikia Machi 31 mwaka huu ambapo wakimbizi waliokuwa wakihifadhiwa kwenye kambi hiyo watarudishwa kwao nchini Burundi.

Kutokana na hali hiyo Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa idadi kubwa ya wakimbizi wa Burundi wanarudi kwao lakini wapo ambao wamekuwa wakitoroka na kuishi mkoani humo isivyo halali hivyo serikali imeamua kufanya operesheni hiyo ziwani na nchi kavu ili kuhakikisha inasafisha viashiria vyote vya uhalifu na uvunjifu wa amani.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI