Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Urusi, tarehe 03 Aprili 2026, zimesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya uchukuzi, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha maendeleo ya miundombinu na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu kati ya nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yalisainiwa pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Uchukuzi na Usafirishaji uliofanyika tarehe 03 Aprili 2026 jijini St. Petersburg, Urusi, yakihusisha Wizara ya Uchukuzi ya Tanzania na Wizara ya Uchukuzi ya Shirikisho la Urusi. Kwa upande wa Urusi, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Andrey Nikitin, alisisitiza utayari wa nchi yake kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika sekta ya uchukuzi, akibainisha kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa wakati wa Mkutano wa Russia - Africa 2023.
Aidha, alieleza dhamira ya Urusi kuendeleza ushirikiano wa kiufundi, uwekezaji katika miundombinu ya kisasa, pamoja na kushiriki katika miradi ya kimkakati itakayochangia maendeleo ya sekta ya uchukuzi nchini Tanzania.
Akizungumza kuhusu makubaliano hayo, Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya uchukuzi kwa kushirikiana na mataifa yenye uzoefu na teknolojia ya kisasa.
Alisema kupitia makubaliano hayo, Tanzania inalenga kujenga ushirikiano wa kiufundi utakaowezesha kubadilishana utaalamu, kutoa mafunzo, na kuhamisha teknolojia, ili kuongeza ufanisi wa miundombinu ya uchukuzi na kuiwezesha nchi kuwa kitovu cha usafirishaji katika ngazi ya kikanda.
Aidha, Prof. Mbarawa alibainisha kuwa ushirikiano huo utafungua fursa zaidi za uwekezaji, utafiti na ubunifu katika miradi ya kimkakati, pamoja na kuimarisha uwezo wa rasilimali watu katika sekta ya uchukuzi.
Kwa ujumla, makubaliano haya yanatarajiwa kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi, hususan katika maendeleo ya sekta ya uchukuzi.



.jpeg)
.jpeg)




0 Comments