Header Ads Widget

UTPC: TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA JAB KUIMARISHA UANDISHI WENYE TIJA NCHINI

 


Na Matukio Daima Media

Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Keneth Simbaya, amesema umoja huo utaendelea kushirikiana kwa karibu na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) katika kuhakikisha taaluma ya habari nchini inaendelea kuzingatia maadili, weledi na uzalishaji wa habari zenye tija kwa maendeleo ya jamii.

Simbaya alisema ushirikiano huo ni sehemu ya dhamira ya UTPC ya kuona waandishi wa habari wanakuwa nguzo muhimu katika kuelimisha, kuhabarisha na kuhamasisha maendeleo ya wananchi kupitia kazi zao za kila siku.

Alitoa kauli hiyo leo alipoungana na viongozi wa Iringa Press Club (IPC) kwenda kutoa pole kwa mlezi wa klabu hiyo, Salim Asas, kufuatia kifo cha baba yake mdogo, Jaffar Abri. Simbaya, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya IPC, alisema pamoja na lengo la kutoa pole kwa familia hiyo, walipata nafasi ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya tasnia ya habari nchini.


Akizungumza katika hafla hiyo, Simbaya alisema UTPC itaendelea kufanya kazi kwa karibu na JAB kuhakikisha waandishi wa habari wanazingatia misingi ya taaluma na kuandika habari zinazochangia maendeleo ya Taifa badala ya taarifa zisizo na manufaa kwa jamii.


“Tunataka kuona waandishi wa habari wanaendelea kutumia kalamu zao kuelimisha wananchi, kuibua hoja za maendeleo na kuhamasisha uwajibikaji. Huo ndiyo mwelekeo wa UTPC kwa kushirikiana na JAB katika kuijenga tasnia ya habari yenye heshima na mchango mkubwa kwa jamii,” alisema Simbaya.

Alisema habari zenye tija zina nafasi muhimu katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya maendeleo, afya, elimu, uchumi, utawala bora na huduma za kijamii, hivyo waandishi wanapaswa kutambua uzito wa jukumu walilonalo.

Aidha, Simbaya alisema UTPC inaendelea kuthamini mchango wa wadau mbalimbali waliokuwa mstari wa mbele kusaidia ukuaji wa tasnia ya habari nchini, akiwemo Salim Asas ambaye amesema ameendelea kuwa mdau muhimu katika kuwawezesha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Kwa mujibu wa Simbaya, mchango wa Asas katika maendeleo ya IPC na tasnia ya habari kwa ujumla umechangia kukuza uwezo wa waandishi wa habari na kuimarisha mazingira ya kazi zao.

“Tunatambua mchango mkubwa wa wadau wetu. Watu kama Salim Asas wameendelea kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya tasnia ya habari nchini. Ushirikiano wao umetuwezesha kuendelea kujenga uwezo wa waandishi na kuimarisha klabu za waandishi wa habari,” alisema.

Simbaya pia alisema changamoto ya uandishi holela imeanza kupungua kutokana na juhudi zinazofanywa na JAB kupitia mfumo wa ithibati pamoja na kusimamia maadili ya taaluma ya habari.

Alisema hatua hizo zimechangia kuongeza uwajibikaji miongoni mwa waandishi wa habari na kuimarisha ubora wa taarifa zinazotolewa kwa umma.

“Leo tunaona mabadiliko makubwa ukilinganisha na miaka iliyopita. Waandishi wengi wanazingatia maadili ya taaluma, na hiyo ni mafanikio yanayotokana na ushirikiano uliopo kati ya UTPC na JAB,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Iringa Press Club (IPC), Frank Leonard, alisema klabu hiyo imeendelea kupata mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya viongozi wake, wanachama na mlezi wa klabu hiyo, Salim Asas.

Leonard alisema viongozi wa IPC waliona ni muhimu kufika nyumbani kwa Asas ili kumpa pole kufuatia msiba uliompata, ikiwa ni sehemu ya kuonyesha mshikamano na kuthamini mchango wake katika maendeleo ya klabu hiyo.

“Tumekuja kama familia. Mlezi wetu amekuwa bega kwa bega na IPC kwa muda mrefu na ametusaidia katika nyanja mbalimbali. Katika kipindi hiki kigumu tuliona ni wajibu wetu kuwa naye pamoja,” alisema Leonard.

Leonard, ambaye pia ni Kaimu Rais wa UTPC, alisema pamoja na changamoto mbalimbali zinazolikabili shirika hilo, hususan baada ya baadhi ya wafadhili wake kujiondoa, bado viongozi wanaendelea kutafuta njia mbadala za kuhakikisha shughuli za klabu za waandishi wa habari zinaendelea bila kuyumba.

Alisema UTPC imejipanga kuendelea kujenga uwezo wa waandishi wa habari kupitia mafunzo, ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha tasnia ya habari inaendelea kukua na kukidhi mahitaji ya jamii.

“Changamoto zipo, lakini hatutakata tamaa. Tunaendelea kupambana kuhakikisha klabu za waandishi wa habari zinaendelea kufanya kazi zake kwa ufanisi na waandishi wanapata fursa za kujiendeleza kitaaluma,” alisema.

Aliongeza kuwa jukumu la msingi la vyombo vya habari ni kuitumikia jamii kwa kutoa taarifa sahihi, kuibua changamoto zinazowakabili wananchi na kusaidia kujenga uwajibikaji katika taasisi za umma na binafsi.


Naye mlezi wa Iringa Press Club, Salim Asas, aliwashukuru viongozi wa UTPC na IPC kwa kufika nyumbani kwake kutoa pole kwa familia kufuatia msiba huo.

Asas alisema kitendo hicho kinaonyesha mshikamano mkubwa uliopo kati ya viongozi wa tasnia ya habari na wadau wake, huku akisisitiza kuwa umoja huo unapaswa kuendelea kuimarishwa kwa manufaa ya sekta ya habari.

Aidha, alipongeza kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari nchini, akisema katika kipindi cha sasa kumekuwa na maboresho makubwa katika namna habari zinavyoandaliwa na kuwasilishwa kwa umma.


Alisema anaendelea kushuhudia mabadiliko makubwa katika tasnia hiyo kutokana na jitihada zinazofanywa na UTPC pamoja na JAB kusimamia maadili, weledi na misingi ya taaluma ya habari.

Asas, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika sekta mbalimbali, hivyo vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo.

Alisema habari zenye tija zinasaidia wananchi kuelewa kazi zinazofanywa na Serikali, kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa.


“Serikali ya chama cha mapinduzi (CCM)chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan  inaendelea kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali. 

Vyombo vya habari vikijikita katika kuhabarisha wananchi kuhusu maendeleo hayo kwa kuzingatia ukweli na weledi, vitakuwa vinatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa,” alisema Asas.


Aliwataka waandishi wa habari kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma, sheria za nchi na maslahi ya umma, huku wakitumia kalamu zao kama chombo cha kuhamasisha maendeleo, kuimarisha uwajibikaji na kujenga jamii yenye uelewa mpana wa masuala mbalimbali ya kitaifa.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI