Samwel Mwanga,Meatu
MWENGE wa Uhuru mwaka 2026 unatarajiwa kuzindua, kuweka mawe ya msingi, kukagua na kufungua jumla ya miradi 40 yenye thamani ya Sh 84.3 bilioni katika Mkoa wa Simiyu.
Miradi hiyo inayotekelezwa katika sekta za elimu, afya, maji, barabara, maendeleo ya jamii na sekta binafsi ipo katika halmashauri za wilaya za mkoa huo ambazo ni Meatu,Maswa,Itilima,Bariadi,Busega na halmashauri ya mji wa Bariadi.
Mwenge huo umepokelewa rasmi leo Julai 26, 2026 katika Kijiji cha Bukundi, Wilaya ya Meatu, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendegu, kuukabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, tayari kwa mbio zake ndani ya mkoa huo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Mwang'onda, amesema Mwenge wa Uhuru unaendelea kuwa alama ya uzalendo, umoja na chachu ya maendeleo kwa Watanzania.
"Mwenge wa Uhuru unahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, kulinda miradi ya umma na kuimarisha uzalendo pamoja na uwajibikaji," amesema
Kwa mujibu wa ratiba ya mbio hizo Mwenge wa Uhuru katika mkoa huo utazindua miradi 11, utaweka mawe ya msingi kwenye miradi 14, utakagua na kuona miradi 11, huku ukifungua miradi minne, na kufanya jumla ya miradi 40 itakayopitiwa katika halmashauri zote za mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amesema ujio wa Mwenge wa Uhuru ni fursa ya kuonyesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi na kuwataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo.
Amesema serikali itaendelea kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa viwango vinavyokusudiwa na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mkazi wa Meatu, John Nyanza, amesema miradi inayopitiwa na Mwenge wa Uhuru imekuwa ikichochea uwajibikaji kwa watendaji na kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo.
"Tunatarajia Mwenge utakagua miradi kwa umakini ili ile yenye kasoro ibainishwe mapema na wananchi wapate huduma bora," amesema.
Naye Maria Mwananjile mkazi wa Bukundi, amesema ujio wa Mwenge wa Uhuru umeongeza hamasa kwa wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo.
"Tunafurahi kuona miradi ya maji, afya na elimu ikipewa kipaumbele. Hii inaonyesha maendeleo yanawafikia wananchi wa kawaida," amesema.
Kwa upande wake, Juma Matekele wa kijiji cha Nkoma wilaya ya Meatu amesema sekta binafsi pia inanufaika na Mwenge wa Uhuru kwa kuwa miradi yake hutambulika na kuhamasisha uwekezaji.
"Tunaomba miradi hii ilindwe baada ya uzinduzi ili iendelee kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu," amesema.
Kauli mbiu ya Mwenge wa uhuru mwaka huu ni Tanzania ni yetu sote,tushirikiane kwa pamoja kuleta maendeleo.
Mwisho








0 Comments