Jamaa za wale wanaosema walilaghaiwa kupigania Urusi wamekuwa wakiitaka serikali ya Kenya kuingilia kati.
Wakenya 16 wametoweka nchini Urusi baada ya kujiunga na jeshi la nchi hiyo, na wengine 47 wamerejea nyumbani kutoka vitani nchini Ukraine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi ameimbia kikao cha kamati ya Bunge la Seneti.
Wengine 38 kwa sasa wako katika hospitali tofauti za Urusi chini ya vizuizi vya ufikiaji Mudavadi aliongeza kusema.
Idadi ya Wakenya waliotoweka nchini Urusi imeongezeka kutoka 10 hadi 16 ndani ya saa 24 zilizopita.
Bado haijabainika ikiwa wamefariki au wako hai.
Waziri huyo pia alikadiria kuwa Wakenya 165 wanashiriki kikamilifu katika operesheni za kijeshi, na kufanya jumla ya walioshiriki katika mzozo wa Ukraine kufikia zaidi ya 250.
Mudavadi alisema idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi.
Aliongeza kuwa Wakenya wawili wanazuiliwa nchini Ukraine kama wafungwa wa kivita.
Mudavadi pi alisema walioajiriwa wametia saini kandarasi za kuhudumu kama maafisa wa usafirishaji au kufanya majukumu ya kivita.
"Kinyume na ripoti zilizopo, Wakenya wengi walijiunga na jeshi la Urusi kwa hiari," Mudavadi aliambia kamati ya wabunge.
Baadhi ya mashirika yenye makao makuu nchini Kenya, Urusi, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu yalihusika na usajili huo, kwa mujibu wa waziri Mudavadi.
Kenya imeanzisha uchunguzi kuhusu usajiliwa kwa raia wake kupigana vita nchini Ukraine kinyume cha sheria.
MWISHO.





0 Comments