Header Ads Widget

RC MAKAME- ATAKAYEZUA TAHARUKI YA KUPOTEZA NYETI TUTARUKA NAYE

 



-Awatoa hofu wananchi watakiwa kuchapa kazi

Na Moses Ng’wat, Tunduma.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, leo Aprili 3, 2026 amelazimika kufanya ziara maalum ya kuzungumza na wananchi  katika maeneo mbalimbali ya mji wa Tunduma, Wilayani Momba kwa lengo la kutuliza hali ya taharuki iliyozuka kufuatia madai ya vitendo vya wizi wa nyeti za wanaume au  nyeti zao kusinyaa na kuwa ndogo kama ya mtoto.

Akizungumza katika eneo la Kilimanjaro na Kisimani Mjini humo, Rc Makame amelaani vikali matukio hayo na kusisitiza kuwa serikali haitavumilia vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia na kwamba yeyote atakayezua  taharuki atakamatwa.

Makame amesema serikali imepokea taarifa za kuongezeka kwa hofu hiyo, hali inayodaiwa kusababisha baadhi ya wananchi kupoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa na kuendelea kupatiwa matibabu hospitalini.

Amesema si jambo linalokubalika kwa wananchi kuishi kwa hofu katika eneo muhimu la kibiashara kama Tunduma, akisisitiza kuwa kila Mtanzania ana haki ya kuishi kwa amani na usalama bila vitisho vya aina yoyote, iwe ni vya kweli au uzushi unaochochea vurugu.

Makame amekemea vikali vitendo vya kujichukulia sheria mkononi vinavyochochewa na imani za kishirikina, akieleza kuwa hali hiyo inarudisha nyuma jitihada za maendeleo na kuchafua taswira ya mkoa huo ambao ni lango muhimu la biashara nchini.

"Hali hii inachafua taswira ya mkoa wetu na niseme mtu yeypte atakajaribu kuzua  taharuki ya kupoteza nyeti tutaruka naye" amesema Makame.

Aidha, Makame amewataka viongozi wa serikali za mitaa kushiriki kikamilifu katika kudhibiti hali hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya dola, huku akionya kuwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria bila upendeleo.

Vile vile amesema serikali mkoani humo inaendelea na  operesheni ya kuwabaini wale wote wanajihusisha na vitendo hivyo na kuahidi kuwa hakuna mtu atakayesalimika iwapo atahusishwa na matukio hayo.

"Wanaume wenzangu niwahakikishie endeleeni kuchapa kazi bila kuwa na hofu...pia nyie akina mama naomba muwaruhusu waume zenu wakafanye kazi na watarudi wakiwa salama na nyeti zao" amesema Makame.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, akizungumza katika mkutano huo, amesema hadi sasa watu wanne wamepoteza maisha na wengine wanne wakiendelea kupatiwa matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kufuatia matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi, huku watu 29 wakishikiliwa kwa kuhusika na matukio hayo ya kujichukulia sheria mkononi.

Senga ametolea mfano wa tukio lililotokea Aprili 2, 2026 katika mji wa Vwawa, Wilayani Mbozi ambapo dereva wa bajaji alijeruhiwa na kulazwa hospitalini, akieleza kuwa chanzo kilikuwa ni mgogoro wa madai ya fedha baina yake na mwenzake, lakini baadaye tukio hilo likageuzwa kuwa madai ya kuguswa na kuanza kushambuliwa.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI