Header Ads Widget

TFS YATOA MICHE 500, YAONGOZA MAPAMBANO YA UHIFADHI BWAWA LA MINDU

 


Na Mwandishi Wetu, Morogoro


MOROGORO — Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kupitia Kituo cha Uzalishaji Mbegu za Miti Morogoro, umetoa miche 500 ya miti ya midodoma na kushiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji miti katika hifadhi ya chanzo cha maji cha Bwawa la Mindu, ikiwa ni juhudi za kulinda usalama wa maji kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro na maeneo jirani.

Zoezi hilo la pamoja limewakutanisha watumishi wa umma, wastaafu kutoka taasisi mbalimbali pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), likiwa na lengo la kurejesha na kuhifadhi vyanzo vya maji vinavyotegemewa na zaidi ya wakazi 500,000.

Akizungumza kwa niaba ya Mhifadhi Mkuu wa Kituo cha Uzalishaji Mbegu za Miti Morogoro, Mhifadhi Mwandamizi (SCO) Helman Ndanzi amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa TFS katika kuimarisha uhifadhi wa mazingira, hususan katika maeneo nyeti ya vyanzo vya maji.

Amesisitiza kuwa uhifadhi wa mazingira haupaswi kuachwa kwa taasisi moja pekee bali unahitaji ushirikiano wa wadau wote, akibainisha kuwa TFS itaendelea kusambaza miche bora na kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha juhudi hizo zinakuwa endelevu.

Kwa upande wake, Meneja wa Mazingira na Usafi wa Mazingira kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), Mhandisi Hafidhi Lacha amesema zoezi hilo linaendana na maadhimisho ya Sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akieleza kuwa upandaji miti ni nguzo muhimu katika kulinda vyanzo vya maji.

“Uwepo wa miti katika maeneo ya vyanzo vya maji unasaidia kuhifadhi unyevunyevu wa ardhi, kuzuia mmomonyoko na kuhakikisha upatikanaji wa maji unaendelea kuwa wa uhakika kwa wananchi,” amesema.

Naye Diwani wa Viti Maalum (CCM) wa Kata ya Maghorofani, Immaculate Mhagama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wauguzi Wastaafu, ametoa wito kwa jamii na makundi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kampeni za upandaji na utunzaji wa miti ili kulinda mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema ushiriki wa wananchi ni nguzo muhimu katika kufanikisha juhudi za uhifadhi na kwamba kila mmoja ana wajibu wa kutunza miti inayopandwa ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya yaliyokusudiwa.

Zoezi hilo linaakisi dhamira ya Serikali kupitia TFS na wadau mbalimbali katika kuhakikisha rasilimali za misitu na maji zinalindwa kwa manufaa ya maendeleo endelevu ya taifa.














Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI