RC Kheri James Azindua Usajili wa Mbio za Great Ruaha Marathon 2026 NA MATUKIO DAIMA MEDIA IRINGA MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amezindua rasmi usajili wa mbio za Great Ruaha Marathon zinazotarajiwa kufanyika mwezi Julai mwaka huu. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kheri aliwataka wananchi wa Iringa na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo, akisisitiza umuhimu wake katika kukuza utalii na uchumi wa eneo hilo. Alibainisha kuwa mbio hizo zimekuwa na mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake, na zimechangia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Iringa na Tanzania kimataifa. Aidha, alitoa wito kwa wadau kuendelea kuzitumia mbio hizo kama jukwaa la kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kutangaza huduma mbalimbali. Awali, Rais na Mkurugenzi wa taasisi ya Sustainable Youth Development Partnership (SYDP), Edward Millinga, alipongeza mchango wa vyombo vya habari mkoani Iringa katika kuhamasisha tukio hilo. Pia aliomba ushirikiano wa serikali ya mkoa katika kupamba mji wa Iringa ili kuvutia washiriki wengi zaidi. Millinga alisema kuwa mwaka huu wanatarajia kupokea washiriki wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi. Alifafanua kuwa Great Ruaha Marathon ni tukio la kila mwaka linalolenga kuwakutanisha wanariadha, wanaharakati wa mazingira na jamii kwa ujumla, kwa lengo la kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, kuwawezesha vijana na kukuza utalii endelevu. Aliongeza kuwa mbio hizo zina mchango mkubwa katika kulinda Mto Mkuu Ruaha pamoja na mfumo wa ikolojia wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambao ni muhimu kwa bioanuwai, wanyamapori na ustawi wa jamii zinazozunguka eneo hilo. Kwa upande wake, Mratibu wa mbio hizo, Hamim Kilahama, alisema maandalizi yanaendelea vizuri huku wakitarajia ushiriki mkubwa wa wadau mbalimbali. Alisisitiza kuwa tukio hilo si la kawaida bali ni sherehe ya kipekee inayochanganya utalii, mazingira na afya. “Mbio hizi ni za kipekee kwa sababu zinafanyika ndani ya hifadhi ya taifa, jambo linalozifanya kuwa miongoni mwa mbio chache duniani zinazofanyika katikati ya mazingira ya wanyamapori,” alisema Kilahama. Aliongeza kuwa tukio hilo linaendelea kuiweka Iringa katika ramani ya dunia kama kitovu cha utalii wa mazingira na michezo. Waandaaji wamewahimiza Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi kuthibitisha ushiriki wao kupitia namba ya simu +255 673 112 753 au kwa kutembelea tovuti rasmi ya mbio hizo.





































0 Comments