Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Kituo cha Uzalishaji wa Mbegu za Miti, wameshiriki uzinduzi wa mradi wa kuhifadhi mazingira unaotekelezwa na Shirika la UECO – Unganisha Environmental Conservation kwa kushirikiana na mradi wa Imarika chini ya Mtandao wa PELUM Tanzania.
Uzinduzi huo umefanyika tarehe 17 Aprili 2026 katika Kata ya Mkundi, Manispaa ya Morogoro, ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Mheshimiwa Mussa Kilakala.
Katika uzinduzi huo, jumla ya mizinga 50 ya kisasa iligawiwa kwa vikundi vya vijana na wanawake kutoka mitaa inayozunguka Mlima wa Mguruwandege ambayo ni Mawasiliano, Kilongo, Kilongo B na Mguruwandege, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha wananchi kiuchumi sambamba na kuhifadhi mazingira.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Kilakala alisisitiza umuhimu wa jamii kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira kwa kutumia mbinu endelevu kama ufugaji nyuki na upandaji miti, ambazo huchangia kulinda vyanzo vya maji na bioanuwai huku zikitoa kipato kwa wananchi.
Akimwakilisha Mhifadhi Mkuu wa Kituo cha Uzalishaji Mbegu za Miti, Mhifadhi Herman Ndazi alisema TFS itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za miti na kuhamasisha upandaji miti katika maeneo ya hifadhi na nje ya hifadhi ili kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii ni nguzo muhimu katika kufanikisha juhudi za uhifadhi wa misitu na mazingira kwa ujumla.
Mradi huo unalenga kuimarisha uhifadhi wa Mlima wa Mguruwandege kwa kuwajengea uwezo wananchi katika shughuli mbadala za kiuchumi ambazo haziharibu mazingira, hivyo kuchangia maendeleo endelevu ya jamii zinazouzunguka mlima huo.


.jpg)















0 Comments