Fadhili AbdallahKigoma
SHIRIKA la uwakala wa meli Tanzania (TASAC) na wadau wa usafiri na usafirishaji majini mkoa Kigoma wamekutana kujadili ongezeko la nauli kwa vyombo vya usafirishaji majini kuendana na ongezeko la bei ya mafuta iliyotokea hivi karibuni.
Katika mkutano huo Mkurugenzi wa udhibiti uchumi wa TASAC Makao makuu, Nahson Sigalla aliwasilisha pendekezo la kupandisha bei ya nauli kwa asilimia 23.7 ili kuwezesha wasafirishaji hao kukabiliana na ongezeko la mafuta ambapo pendekezo hilo linatokana na ukokotoaji uliofanywa na TASAC kuhakikisha wadau wote wanasafiri na kusafirisha bila upande mmoja kuathirika na ongezeko hilo.
Alisema kuwa kutokana na pendekezo hilo wametoa muda kuanzia April 16 hadi 24 mwaka huu kwa wadau wote wakiwemo wamiliki, waendeshaji, abiria kutoa maoni yao ambayo yatachakatwa na mwisho kutoa bei ambayo itakuwa na mslahi kwa pande zote bila kumuumiza abiria, msafirishaji au mmiliki wa chombo cha usafirishaji majini.
Wakizungumza katika mkutano huo wadau wa usafirishaji majini akiwemo Mwenyekiti wa Umoja wa wamiliki wa maboti Kigoma (UWAMAKI), Abdul Ally ambaye alisema kuwa kiwango kilichopendekezwa na TASAC ni kidogo ukilinganisha na kiwango cha kupanda kwa bei ya mafuta.
Ally alisema kuwa kwa Zaidi ya miaka 10 hawajapandisha bei lakini mafuta yalipanda bei kutoka 2370 na kufikia shilingi 4000 kwa sasa hivyo kiwango cha asilimia 23.7 ni kidogo hivyo wakataka kiongezwe maradufu.


.jpeg)




0 Comments