NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,NJOMBE
Maofisa wawili wa wakala wa misitu Tanzania TFS wilaya ya Makete mkoani Njombe wamehukumiwa Kifungo cha miaka miwili jela ama kulipa faini ya shilingi laki tano kila mmoja baada ya kukutwa na hatia ya kuomba na kupokea Rushwa ya mil 8 kwa Yuda Male mkazi wa kijiji cha Mfumbi kata ya Mfumbi wilayani hapo ambaye ni mfugaji baada ya kuingiza mifugo katika Msitu wa asili wa serikali wa Chimala.
Akisoma mashitaka katika mahakama ya wilaya ya Makete Aprili 16, 2026 Hakimu mkazi Mfawidhi Mwandamizi mahakama hiyo Irvan Msacky amesema mshitakiwa Thadeus James Mtui(31) mhifadhi TFS Matamba na Florian Giliad Kilango(33) afisa wa TFS wilaya ya Makete
kwa nyakati tofauti watumishi hao walichukua rushwa kwa mfugaji huyo baada ya kumkuta akilisha mifugo katika Msitu wa asili wa serikali kitendo ambacho ni kinyume na kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sura ya 329 marejeo ya Mwaka 2024.
Katika mashtaka hayo ambayo yalifunguliwa na taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Makete, Mwendesha mashitaka wa TAKUKURU mkoa wa Njombe Daniel Mono ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili iwe fundisho
Washitakiwa hao wamekiri kutenda makosa hayo ya kuomba na kupokea rushwa na ndipo wakahukumiwa na mahakama hiyo, lakini ili kukwepa kifungo cha miaka miwili jela wakalipa faini ya shilingi laki tano kila mmoja.
Washitakiwa Thadeus James Mtui na Florian Gilliad Kilango walichukua rushwa ya kwanza mnamo tar 1/11/2025 kiasi cha Mil 2 baada ya kukamata mifugo ya Yuda Male na kisha kuchukua rushwa nyingine kiasi cha mil 6 mnamo 31/1/2026 baada ya kushika tena mifugo ya mfugaji huyo katika Msitu uleule wa asili wa Chimala uliopo kijiji cha Mfumbi kata ya Mfumbi wilayani Makete.
Licha kukiri kosa lao na kisha kulipa faini,Mahakama imeagiza wawili hao pia kurejesha fedha yote waliyochukua kwa mfugaji huyo kiasi cha shilingi milioni 8 ambaye inaelezwa aliamua kuripoti katika vyombo vya dola kutokana usumbufu alioendelea kuupata ili hali aliwapa rushwa watumishi hao.
Imeelezwa mahakamani hapo kwamba kwa sasa serikali imekuwa ikihimiza utunzaji wa mazingira, hivyo kwa kuwa maafisa hao wamepewa dhamana na serikali ya kuhakikisha wanalinda misitu yake hivyo kitendo cha kujihusisha na rushwa hakikubaliki hivyo adhabu hiyo imetolewa ili iwe fundisho kwa washitakiwa na wengine wenye nia ya kufanya vitendo hivyo.







0 Comments