Arusha / Nairobi, 31 Machi 2026
Kulinda na kurejesha bioanuwai si hatua ya hiari katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi bali ni wajibu wa kisheria unaotokana na haki za binadamu, WWF imesema katika wasilisho la amicus curiae lililowasilishwa kwa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kuhusu wajibu wa nchi katika kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi.
Wasilisho hili linakuja wakati Mahakama ya Afrika inakuwa mahakama ya tatu duniani au kikanda kuombwa kutoa uamuzi wa kihistoria kuhusu wajibu wa nchi katika janga la mabadiliko ya tabianchi.
Ingawa maoni ya ushauri si ya lazima kisheria, maamuzi ya hivi karibuni ya mahakama za kimataifa na kikanda yamekuwa na uzito mkubwa wa kimaadili na kisheria, yakitoa ufafanuzi wa kipekee kuhusu wajibu wa nchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na mfumo thabiti wa kuwawajibisha wachafuzi.
Kwa upande wa Afrika, ombi la maoni ya ushauri linaweka mkazo mkubwa kwenye haki za binadamu, na WWF inaeleza kuwa ulinzi wa bioanuwai unapaswa kutambuliwa kama sehemu ya haki hizo.
“Mabadiliko ya tabianchi na upotevu wa bioanuwai ni migogoro isiyotenganishwa,” alisema Laurent Some, Mkurugenzi wa Kanda wa WWF Afrika ukanda wa Kongo.
“Asili si tu ipo mstari wa mbele kupokea athari mabadiliko ya tabianchi, bali pia ni mshirika mkubwa wa binadamu katika kudhibiti Athari hizo iwapo hatua sahihi zitachukuliwa.
Kushindwa kulinda bioanuwai kunadhoofisha juhudi za kukabiliana na Athari za mabadiliko ya tabianchi na kunatishia haki na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.
”Afrika ni makazi ya zaidi ya robo ya bioanuwai ya dunia, ikijumuisha misitu, ardhi oevu, nyanda za majani na mifumo ya ikolojia ya baharini yenye umuhimu wa kimataifa. Mifumo hii inasaidia usalama wa chakula, ajira, afya, upatikanaji wa maji na maendeleo ya kiuchumi kwa mamilioni ya watu.
Pia ina jukumu muhimu katika kupunguza na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kufyonza na kuhifadhi hewa ukaa, kudhibiti hali ya hewa, na kulinda jamii dhidi ya majanga yanayohusiana na tabianchi kama mafuriko, ukame na mawimbi makubwa ya bahari.
Wasilisho la WWF linaonyesha hali ya kutia wasiwasi. Kulingana na Ripoti ya Living Planet ya WWF ya mwaka 2024, idadi ya wanyamapori wanaofuatiliwa barani Afrika imepungua kwa asilimia 76 tangu mwaka 1970, hali inayosukuma mifumo ya ikolojia kuelekea kwenye viwango hatarishi na visivyoweza kurekebishwa.
Upotevu huu unaoongezeka, unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na shinikizo nyingine, tayari unadhoofisha uwezo wa Afrika wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Wasilisho hili linaendeleza hoja zilizotolewa na WWF kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mwaka 2024, ambapo iliitaka mahakama hiyo kutambua wajibu wa kisheria wa nchi kulinda mifumo ya ikolojia inayodhibiti tabianchi pamoja na bioanuwai, sambamba na wajibu wao wa kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.
Katika maoni yake ya kihistoria yaliyotolewa Julai 2025, ICJ ilitambua wazi wajibu wa nchi kuepuka madhara ya tabianchi na kulinda asili kama sehemu muhimu ya mfumo wa tabianchi ikithibitisha uhusiano wa msingi kati ya mifumo ya ikolojia yenye afya, utulivu wa tabianchi na ustawi wa binadamu.
WWF inaeleza kuwa kanuni hizi zinatumika kwa nguvu zaidi katika muktadha wa Afrika kwa mtazamo wa haki za binadamu, kutokana na utegemezi mkubwa wa bara hili kwa asili na kukumbwa zaidi na hatari za tabianchi.
WWF inasisitiza kuwa mchakato huu kimsingi unahusu haki ya tabianchi.
Kwa kufafanua wajibu wa kisheria wa nchi, mahakama inaweza kusaidia kuhamisha mjadala wa tabianchi kutoka kwenye siasa kwenda kwenye wajibu wa kisheria na haki za binadamu na hivyo kuzipa jamii za Afrika zana imara zaidi za kudai hatua, uwajibikaji na haki.WWF inaongeza kuwa kulinda bioanuwai ni muhimu katika kulinda haki mbalimbali za binadamu, zikiwemo haki ya chakula, maji, afya, maisha na kutobaguliwa.
Uharibifu wa mifumo ya ikolojia na upotevu wa bioanuwai unaathiri zaidi watu wa asili, wanawake, watoto na jamii zilizo katika mazingira magumu, na pia unahatarisha vizazi vijavyo.
Aidha, WWF inaelekeza kwenye mifumo ya kisheria na sera za Afrika, ikiwemo Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Mkataba wa Afrika wa Uhifadhi wa Asili na Rasilimali Asilia, ambayo inatambua wajibu wa nchi kulinda mazingira na rasilimali asilia kwa maendeleo endelevu.
“Kwa Afrika, kuhimili na kujenga ustahimilivu lazima viwe kipaumbele,” alisema Yvonne Godo, Mkurugenzi wa Kanda wa WWF Afrika kwa Afrika Mashariki na Kusini.
“Kulinda na kurejesha mifumo ya ikolojia yenye bioanuwai ni muhimu sana katika kusaidia jamii kuhimili athari za tabianchi, kuimarisha ustahimilivu na kulinda haki za binadamu barani kote.
”WWF inahitimisha kuwa nchi za Afrika zinaweza tu kutimiza wajibu wao wa haki za binadamu na kushughulikia ipasavyo mzozo wa tabianchi ikiwa zitachukua hatua za haraka, zinazoongozwa na sayansi na zenye uratibu katika kuhifadhi na kurejesha bioanuwai.
Hatua hizo, WWF inasema, ni wajibu wa kisheria na pia ni sharti muhimu kwa tabianchi thabiti, mustakabali unaoishi na haki ya watu wa Afrika kuwa na mazingira bora yanayofaa maendeleo yao.

.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)




0 Comments