Header Ads Widget

ELIMU YA MUUNGANO YAONGEZEWA NGUVU, WANANCHI WAHIMIZWA KUTUMIA FURSA ZA MAENDELEO

Mahitaji ya kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yanaendelea kujitokeza, huku viongozi wakisisitiza kuwa uelewa huo ni chachu ya kufungua fursa za maendeleo kwa pande zote mbili za Muungano.

Akizungumza mkoani Morogoro wakati wa ziara ya kikazi katika wilaya za Morogoro, Mvomero na Kilosa kwenye maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, anasema ipo haja kwa wananchi kuendelea kuelimishwa kuhusu manufaa ya Muungano ili waweze kunufaika kikamilifu na fursa zinazopatikana.

Ameeleza kuwa licha ya changamoto zilizowahi kuikabili Muungano, hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kuzitatua, hali inayochangia kuimarika kwa ushirikiano na mshikamano wa kitaifa.


Katika hatua nyingine, amebainisha kuwa kati ya kero tatu zilizokuwa zinatajwa mara kwa mara, moja tayari imeshapatiwa ufumbuzi, ikiwemo suala la kuruhusu bidhaa ya sukari kutoka Zanzibar kuingia upande wa Tanzania Bara, hatua inayorahisisha biashara na kukuza uchumi.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na sekta mbalimbali ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa wakati.


Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Prof.Adolf Mkenda, amesisitiza umuhimu wa uwekezaji katika sekta ya elimu, akieleza kuwa miundombinu bora ya elimu ni msingi wa maendeleo endelevu ya taifa.

Wananchi wa Mkoa wa Morogoro


wameeleza kuwa Muungano umeendelea kuwa na manufaa katika maisha yao ya kila siku, hususan katika biashara, elimu na uhuru wa kusafiri na kufanya shughuli mbalimbali kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar anaweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Chuo cha Ualimu Dakawa, anatembelea ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mvomero pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa stendi ya mabasi ya SGR, akisisitiza kuwa miradi hiyo ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma za kijamii.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI