Header Ads Widget

MBUNGE MHANDISI REMBO ASIFU MIAKA 62 YA MUUNGANO AMPONGEZA RAIS DKT SAMIA NA DKT MWINYI KWA KUENZI MUUNGANO

 


Na Matukio Daima Media 

MBUNGE wa viti maalum kutoka mkoa wa Iringa, Mhandisi Fatma Ally Rembo, ameungana na Watanzania wengine kuadhimisha miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akisisitiza umuhimu wa kuulinda na kuuenzi Muungano huo ambao umekuwa nguzo muhimu ya amani, umoja na maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhandisi Rembo alisema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni hazina adhimu iliyojengwa kwa misingi ya mshikamano, uzalendo na maono ya viongozi waasisi, hivyo unahitaji kuendelezwa kwa juhudi za pamoja kutoka kwa kila Mtanzania bila kujali tofauti zao za kijamii, kisiasa au kiuchumi.

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 62 tangu kuanzishwa kwa Muungano huo mwaka 1964, Tanzania imeendelea kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kote kwa namna ilivyoweza kudumisha amani na utulivu wa kudumu. 

Kuwa mafanikio hayo yametokana na misingi imara iliyowekwa na waasisi wa taifa pamoja na juhudi za viongozi waliokuja baadaye.


“Msingi wa Muungano wetu ni umoja na mshikamano. Tunapaswa kujivunia hatua tulizopiga kama taifa na kuendelea kulinda tunu hii kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Mhandisi Rembo.

Aidha, alitoa pongezi kwa waasisi wa Muungano huo kwa maono yao ya mbali yaliyowezesha kuunganishwa kwa mataifa mawili na kuunda taifa moja lenye nguvu.

 Alisema bila uamuzi huo wa kihistoria, huenda Tanzania isingekuwa na nafasi ya kipekee iliyonayo leo katika kudumisha amani na utulivu.

Mbunge huyo pia aliwapongeza viongozi wa sasa wa nchi kwa kuendelea kusimamia na kuimarisha Muungano huo. 


Mhandisi Rembo alimtaja  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Husein Mwinyi, kwa juhudi zao za kuhakikisha Muungano unaendelea kuwa imara na wenye manufaa kwa pande zote mbili.

Hata hivyo alisema  kuwa uongozi wao umeonyesha dhamira ya dhati ya kulinda Muungano na kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwa busara na hekima.

 Kuwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali zinaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, hali inayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mbali na pongezi hizo, Mhandisi Rembo aliwataka Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika kulinda na kudumisha Muungano huo. 


Alisema kuwa jukumu la kuulinda Muungano si la viongozi pekee, bali ni la kila mwananchi anayeitakia mema nchi yake.

“Ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha kuwa Muungano wetu unaendelea kuwa imara. Tujivunie Taifa letu na tushirikiane katika kujenga mustakabali bora zaidi,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa elimu kuhusu historia na umuhimu wa Muungano inapaswa kuendelea kutolewa kwa vijana ili waweze kuelewa thamani yake na kushiriki katika kuulinda. 

Alisema kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa na wana nafasi kubwa ya kuhakikisha kuwa misingi ya Muungano inaendelea kudumu.

Ikumbukwe kuwa maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano yamekuwa fursa ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana pamoja na kuangalia namna bora ya kuendeleza ushirikiano kati ya pande mbili za Muungano. 



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI