Header Ads Widget

WAZIRI NANAUKA AKABIDHI MKOPO WA MILIONI 140 KWA VIJANA MTWARA

 


NA MATUKIO DAIMA MEDIA

MTWARA.Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amekabidhi mkopo wa vijana wenye thamani ya shilingi milioni 140 kwa njia ya vifaa vilivyowekewa bima, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuwawezesha vijana kiuchumi.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na pikipiki 15, bajaji 5 na mikokoteni ya kubebea mizigo maarufu kama “guta” 5, vitakavyowanufaisha vijana wa Mtwara Region. Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa shilingi bilioni 200 zilizotolewa na Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Ugawaji huo umefanyika Machi 2, 2026 wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana Mkoa wa Mtwara, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Stella Maris Mtwara University College.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Nanauka amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha vijana wanapata fursa za kiuchumi kupitia mikopo yenye masharti nafuu, akibainisha kuwa waliopata mkopo huo wataanza kurejesha fedha baada ya miezi mitatu ili kuwapa nafasi ya kujiimarisha kwanza.

“Nimeombwa kukabidhi mikopo kwa vijana katika mfumo wa vifaa ambao mkopo huu utajumlisha pikipiki 15, bajaji 5 na mikokoteni ya kubebea mizigo maarufu kama “guta” 5, zenye thamani ya shilingi Mil 140 zitakazo wanufaisha vijana 40 wanaopatikana katika mkoa huu wa Mtwara na huu ni mwendelezo wa ahadi ambao Dkt Samia suluhu Hassan ameufanya kwa lengo la kuwainua vijana”

Aidha, ametoa wito kwa vijana kote nchini kutumia ipasavyo fursa zinazotolewa na serikali, kutafuta taarifa sahihi na kuzifanyia kazi kwa bidii ili kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, amewahimiza vijana kumuunga mkono Rais Samia katika azma ya kuwakabidhi vijana uchumi wa nchi. Amewataka wanufaika wa vifaa hivyo kuonyesha mfano bora wa matumizi sahihi ya mikopo ili wengine pia waweze kunufaika.

Naye Katibu wa Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Mtwara, Hashimu Ally, ameipongeza serikali kwa kutoa mikopo kwa mfumo wa vifaa badala ya fedha taslimu, akisema hatua hiyo italinda mtaji wa vijana na kuhakikisha vifaa walivyokabidhiwa vinatumika kuzalisha kipato chao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI