Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa matanki 15 ya kuhifadhia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, katika hafla iliyofanyika wilayani Kigamboni Dar es Salaam.
Mradi huo, wenye thamani ya shilingi bilioni 678.6, ni sehemu ya mkakati mpana wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, unaolenga kuongeza ufanisi wake na kushindana kimataifa, pamoja na kuimarisha nafasi yake kama lango kuu la biashara nchini na katika ukanda wa Bahari ya Hindi.
Akizungumza leo, Machi 3, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea mafuta, Rais Samia amebainisha kuwa hali ya dunia kwa sasa tayari imesababisha bei ya mafuta kupanda kwa 13% ndani ya wiki moja tu.
Aidha ameiagiza Wizara ya Nishati kuimarisha akiba ya kimkakati ya mafuta ya taifa ili kuilinda nchi dhidi ya misukosuko ya siasa za kidunia na kupanda kwa bei ya nishati ambapo Kauli hii ya Rais inakuja wakati dunia ikishuhudia mtikisiko mkubwa kufuatia mapigano makali kati ya Israel na Marekani dhidi ya Iran, hali inayozua hofu ya kukatika kwa mnyororo wa usambazaji wa nishati duniani.
“Lakini tumuombe Mungu watu wale wakae juu ya meza wazungumze wakubaliane na hii misukosuko iishe ili dunia irudi katika hali ya kawaida kuendesha uchumi wa nchi zetu. Kwa hiyo ni vyema kutokana na mabadiliko hayo ya siasa za kidunia tukawa na mradi kama huu ili kujihakikishia usalama wa nishati hii ya mafuta”.






0 Comments