Header Ads Widget

OWM YASISITIZA UJUMUISHWAJI WA WATU WENYE ULEMAVU KATIKA MIPANGO YA TAIFA

 

Na Matukio Daima Media  – Dar es Salaam

SERIKALI imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha Watu Wenye Ulemavu wanapata nafasi sawa katika nyanja zote za maendeleo, ikiwa ni pamoja na kijamii, kiuchumi na kisiasa, kupitia sera, sheria na mipango jumuishi inayotekelezwa nchini.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Dkt. Jim Yonazi wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa vyama vya Watu Wenye Ulemavu na mashirika yasiyo ya kiserikali kujadili utekelezaji wa sera, sheria na miongozo ya ujumuishaji nchini.


Amesema hatua kubwa zimeendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma, ambapo Sera ya Taifa ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 pamoja na Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 zimekuwa msingi muhimu wa utekelezaji wa haki na usawa kwa kundi hilo.

“Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa kila sera, mpango na huduma inayotekelezwa nchini inazingatia ujumuishaji wa Watu Wenye Ulemavu tangu hatua ya upangaji, utekelezaji, ufuatiliaji hadi tathmini, ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma,” amesema Dkt. Jim Yonazi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa mawasiliano bora na uratibu imara kati ya Serikali, vyama vya Watu Wenye Ulemavu na mashirika yasiyo ya kiserikali, akibainisha kuwa ushirikiano huo ni msingi muhimu wa kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo.


Amesema ujumuishaji si jukumu la sekta moja pekee, bali ni wajibu wa kila taasisi, kila sekta na kila mdau wa maendeleo. “Tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha huduma zote zinamfikia kila mwananchi kwa usawa,” alisisitiza.

Dkt. Yonazi pia ametoa wito wa kuimarishwa kwa mifumo ya mawasiliano inayowezesha Watu Wenye Ulemavu kupata taarifa kwa urahisi, ikiwemo matumizi ya lugha ya alama, maandishi ya Breli, teknolojia saidizi na mifumo mingine jumuishi.

“Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na vyama vya Watu Wenye Ulemavu pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kutoa huduma za utetezi wa haki, elimu kwa umma, mafunzo ya kujenga uwezo, uwezeshaji kiuchumi, huduma za afya, elimu jumuishi na ushauri wa kitaalamu,” amesema.


Katika hatua nyingine, Dkt. Yonazi amesema kuwa pamoja na jitihada ambazo Serikali imeendelea kuzichukua, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji ushirikiano wa wadau wote.

Amesema changamoto hizo ni pamoja na uelewa usioridhisha kuhusu masuala ya ujumuishaji katika baadhi ya sekta, utekelezaji usiofanana wa sera na sheria, pamoja na changamoto za upatikanaji wa huduma jumuishi zinazokidhi mahitaji ya Watu Wenye Ulemavu.

“Kutokana na hali hiyo, kikao hiki ni muhimu sana kwa kuwa kinatoa fursa ya kujadili kwa kina namna bora ya kuimarisha ujumuishaji wa huduma katika sekta zote.”


Awali, Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Bi. Tungi Mwanjala, ameiomba Serikali kuendelea kuangalia uwezekano wa kuwatambua watoto wa wazazi wenye ulemavu ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo, ikiwemo kupata mikopo ya elimu ya juu kwa urahisi.


Bi.Mwanjala ameeleza kuwa, Serikali imepiga hatua kubwa kwa kukamilisha muongozo na mfumo wa utambuzi wa watu wenye ulemavu, lakini bado kuna haja ya kupanua utambuzi huo kwa watoto wa wazazi wenye ulemavu.


"Tunashukuru Serikali kwa kukamilisha muongozo na mfumo wa kutambua watu wenye ulemavu. Hata hivyo, tunaomba pia watoto wetu watambuliwe kupitia mfumo maalumu utakaowezesha kupata vitambulisho, jambo litakalowarahisishia kupata mikopo ya elimu ya juu na fursa nyingine za maendeleo ikiwamo ajira kwa kuzingatia utaratibu uliopo," amesema.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI