Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi amekutana na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Jaji Blaise Tchikaya na kufanya mazungumzo nae Ofisi kwake jijini Arusha kwa lengo la kujitambulisha kwa Rais huyo ili kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Ofisi hizo mbili.
Dkt. Possi amefika Ofisini kwa Rais wa Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Tchikaya baada ya ufunguzi wa mwaka wa Mahakama hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama hiyo jijini Arusha na uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 ya Mahakama hiyo.
Dkt. Possi amesema kuwa Tanzania kama nchi mwenyeji na kwa kuzingatia majukumu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeona ni muhimu kufika na kujitambulisha, kumpongeza kwa kuwa Rais wa Mahakama hiyo na kumsalimu.
“Ofisi ina jukumu la kuendesha mashauri ya Serikali, utakutana na Ofisi hii katika kuendesha mashauri na Tanzania imekuwa na idadi ya mashauri ambayo yanaendeshwa na Mahakama hii na nimeona nifike tuzungumze ili kukuhakikishia ushirikiano na Ofisi hii kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uendeshaji wa mashauri kwenye Mahakama hii,” amesisitiza Dkt. Possi.
Pia, Dkt. Possi ameongeza kuwa kama nchi mwenyeji yuko tayari kupokea ujumbe kwa niaba ya Serikali ili kuweza kuwasilisha kwa kuwa Ofisi imekuwa inashirikiana na Mahakama hii katika muktadha huo.
Naye Mhe. Jaji Tchikaya, Rais wa Mahakama hiyo amesema kuwa ni kweli mashauri mengi yanayoendeshwa na Mahakama hiyo yanatokea Tanzania na hii inaonesha kuwa uwepo wa Mahakama hii Tanzania inawapa fursa wadau kutumia Mahakama hii baada ya kupita kwenye Mahakama za ndani.
Mhe. Jaji Tchikaya ameongeza kuwa hii inaonesha Tanzania inaruhusu wananchi wake kutafuta na kupata haki kupitia kwenye vyombo vya kimataifa ikiwemo Mahakama hii ambapo ni ushahidi wa utekelezaji wa Mkataba na Itifaki ya Haki za Binadamu wa Umoja wa Afrika.
Katika hatua nyingine, Mhe. Jaji Tchikaya ameomba ushirikiano wa Dkt. Possi na msukumo katika ujenzi wa Ofisi ya Mahakama hiyo ili uweze kukamilika na ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha kuanza kwa ujenzi wa Ofisi ya Mahakama hiyo jijini Arusha.











0 Comments