Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Wanawake wahifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Kituo cha Uzalishaji Mbegu za Miti pamoja na TFS Wilaya ya Mvomero (DFC Mvomero), wameadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto wanaohitaji malezi cha Mission to the Homeless Children kilichopo Mkundi, mkoani Morogoro.
Ziara hiyo iliyofanyika Machi 8, 2026 imelenga kuonesha mshikamano wa wanawake wahifadhi katika kusaidia jamii, hususan makundi yenye uhitaji maalum, sambamba na kuadhimisha mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mary Almas Bakhesha, mmoja wa wanawake wahifadhi kutoka Kituo cha Uzalishaji Mbegu za Miti, alisema maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni fursa muhimu kwa wanawake kuonesha upendo na mshikamano kwa jamii inayowazunguka.
Alisema wanawake hao wameguswa na hali ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho na hivyo kuamua kutumia siku hiyo kuwafariji kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali ikiwemo vyakula, sabuni, nguo na vifaa vingine muhimu kwa matumizi ya kila siku.
Kwa upande wao, wamiliki wa kituo hicho, Bw. na Bi. Robert Simba, walishukuru msaada huo na kueleza kuwa utasaidia kuboresha ustawi wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho.
Walisema ushirikiano wa taasisi na wadau mbalimbali katika kusaidia vituo vya kulelea watoto ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanaopata malezi katika vituo hivyo wanapata mahitaji muhimu kwa ukuaji na maendeleo yao.
Kupitia hatua hiyo, wanawake wahifadhi wa TFS Kituo cha Uzalishaji Mbegu za Miti na TFS Wilaya ya Mvomero (DFC Mvomero) wameonesha kuwa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanaweza pia kuwa jukwaa la kuimarisha mshikamano wa kijamii na kusaidia makundi yenye uhitaji maalum katika jamii.














0 Comments