Na. Mwandishi Wetu, Dar.
SHUJAA wa Sikoseli (Seli mundu) ambaye pia ni Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Jumuiya ya watu wanaoishi na Sikoseli nchini, Bi. Arafa Salim Said ametoa wito kwa Jamii kuendelea Kufanya matendo mema ya kila siku ikiwemo kusaidia wengine na hata kuonesha tabasamu kwani inasaidia katika matendo mema ya kila siku.
Bi. Arafa Said ameyasema hayo katika kongamano maalum lililoandaliwa na Good Deeds Day Tanzania likiwa na lengo kuwajengea uwezo na kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa matendo mema katika kusaidia Jamii.
Akizungumza kando ya kongamano hilo, Bi. Arafa amebainisha: "Napenda kufanya matendo mema kwa sababu katika hii Dunia kila mmoja amekuja na kusudi lake.
Mimi napenda kuwasaidia watu kufikia katika malengo yao. Lakini pia napenda kufanya kazi na taasisi ya Good Deeds Day kwa sababu moja ya nafasi yangu katika maisha kusudi langu la kusaidia Jamii linatimia kupitia wao". Amesema Bi. Arafa Said.
Aidha, katika kongamano hilo, Bi. Arafa Said ameweza kutoa historia yake aliyopitia na harakati mbali mbali za kusaidia Jamii ya watu wenye sikoseli nchini.
“Kama tunavyojua, ili mtoto azaliwe akiwa na ugonjwa wa sikoseli ni lazima arithi vinasaba vya ugonjwa huo kutoka kwa wazazi wote wawili. Inasemekana niligundulika nikiwa na miezi minane tu baada ya kuzaliwa,” amesema Bi. Arafa Said.
Anabainisha kuwa, Kutokana na changamoto ya upungufu wa elimu kuhusu ugonjwa wa sikoseli, Bi. Arafa Said aliamua kujitolea kuelimisha jamii, mashujaa wenzake na walezi kuhusu namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Arafa anatoa wito kwa mashujaa wa sikoseli nchini kuendelea kupambana na hali zao bila kukata tamaa, akisema ugonjwa huo haupaswi kuwa kikwazo cha kutimiza malengo ya maisha.
"Sisi kama Mashujaa wa Sikoseli tunatakiwa kukubali na kuamini kwani maisha hayaishii hapa.
Wito wangu kwa Jamii kujitokeza kupima Sikoseli mapema lakini pia kutowanyanyapaa wagonjwa wa Sikoseli". Amesema Bi Arafa Said.
Good Deeds Day ukiwa ni mwamvuli wa harakati za kujitolea zinazolenga kuchangia maendeleo endelevu kwa kuzingatia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Umoja wa Mataifa, ikiwemo uhifadhi wa mazingira, ustawi wa jamii, usawa wa kijinsia, afya bora, elimu na kupunguza umaskini, kwa lengo la kuleta matokeo chanya na kuboresha maisha ya watu kwa ujumla.
Katika kongamano hilo limewakutanisha washiriki 50 kutoka taasisi mbali mbali, likilenga kutoa muongozo, motisha na maarifa juu ya utekelezaji wa matendo mema katika jamii.
Kwa mwaka 2026, harakati za Good Deeds Day zinaongozwa na kauli mbiu “Tuungane pamoja katika kufanya matendo mema”, sambamba na maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa harakati hizo duniani, zikiwa na kauli mbiu pana zaidi ya “Tuungane kwa pamoja katika kufanya matendo mema kutoka moyoni.”
Kwa mujibu wa muasisi wa Good Deeds Day Tanzania , Doroth Namuhisa, anasema hizi ni harakati za kimataifa zinazohusisha takribani watu milioni 4.5 katika nchi 115, ambapo kila nchi kuanzia mtu binafsi, taasisi, serikali hadi mashirika wanahimizwa kushiriki kufanya matendo mema kila siku.
Imeelezwa kuwa kilele cha maadhimisho ya Good Deeds Day hufanyika kila mwaka tarehe 12 Aprili, siku inayotumika kutambua, kupongeza na kusherehekea jitihada za watu na taasisi zinazojitolea kuboresha maisha ya jamii.
Good Deeds Day ni harakati za kujitolea zinazolenga kuchangia malengo ya maendeleo endelevu, ikiwemo uhifadhi wa mazingira, ustawi wa jamii na kuleta matokeo chanya yanayoboresha maisha ya watu kwa ujumla.
Mwisho.





0 Comments