Watanzania wametakiwa kuendeleza uhifadhi wa Wanyamapori kwa kuwa wanyamapori hao sio tu ni kivutio cha kustaajabisha na kuhusudiwa bali ni rasilimali muhimu katika kulipatia Taifa fedha za kigeni na ni uchumi wa nchi
Akifunga rasmi maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani, Jijini Arusha, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema rasilimali za Misitu na wanyamapori ni urithi na kivutio kinacholiingizia Taifa fedha za kigeni na kusaidia kuinua uchumi wa Nchi.
Dkt. Kijaji amepongeza jitihada za makusudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan zilizowezesha kuendeleza na kuimarika kwa uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii nchini na kuiwezesha kung’ara kinataifa na kujipatia tuzo.
"Utalii hapa nchini, unachangia zaidi ya asilimia 25 ya fedha za kigeni, asilimia 17.1 ya Pato la Taifa na ajira takribani milioni 1.6 zilizo rasmi na zisizo rasmi". Alisema Dkt. Kijaji
Licha ya kuzipongeza taasisi zote za uhifadhi nchini, amezitaka kuendelea kuongeza nguvu katika uhifadhi endelevu wa Maliasili nchini hususani Wanyamapori dhidi ya ujangili na uharibifu mwingine.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Nkoba Mabula, amesema kuwa ofisi yake itasimamia kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa ili kuhakikisha uhifadhi unaendelea kuwa neema kwa watanzania na taifa kwa ujumla.
Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo yenye kaulimbiu "Mimea Dawa na Manukato: Kutunza Afya, Kuhifadhi Urithi na Kuboresha Maisha", Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Dkt. Alexander Lobora amesema, yamelenga kuwakumbusha wananchi kuhusu mchango wa mimea dawa na manukato katika kutunza afya ya binadamu, kudumisha urithi na kuboresha maisha ya jamii na uhifadhi wa Wanyamapori nchini ambao kwa asilimia kubwa wanategemea mimea.











0 Comments