Header Ads Widget

RAIS SAMIA APONGEZWA KWA UONGOZI MAHIRI KATIKA SEKTA YA MALIASILI NA UTALII*


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa uongozi wake mahiri na shupavu katika kuliongoza Taifa la Tanzania, ambapo ameendelea kuimarisha sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya maliasili na utalii nchini.

Pongezi hizo zimetolewa leo, tarehe 08 Machi 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rose Senyamule, alipokuwa akihutubia katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Mbande, Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma.

Mhe. Senyamule amesema kuwa Rais Samia ni mfano wa kuigwa kwa wanawake wote ndani na nje ya nchi, kwani ameonesha uwezo wa kipekee katika uongozi. Ameeleza kuwa katika sekta ya utalii, uongozi wake umeiwezesha Tanzania kushinda tuzo mbalimbali za kimataifa, jambo linalodhihirisha kuwa ni kiongozi mwanamke shupavu na wa kipekee.

“Rais Samia ni mwanamke mahiri sana na analiongoza taifa hili kwa ufanisi mkubwa. Tumeona taifa likipata tuzo mbalimbali kutokana na uongozi wake. Sekta ya utalii imefanikiwa kushinda tuzo tano muhimu; Tanzania inatambuliwa kama kituo bora duniani kwa utalii wa safari na pia  barani Afrika. Aidha, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imetambuliwa kama hifadhi bora duniani, huku Zanzibar ikijulikana kama mahali bora barani Afrika kwa mapumziko ya makampuni (corporate retreat),” amesema Senyamule.

Vilevile, ametumia fursa hiyo kuzipongeza wizara na taasisi zote za Serikali zilizoshiriki katika kilele cha maadhimisho hayo. Amewahimiza wanawake kutoka taasisi hizo kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii, ubunifu na uadilifu ili kulisaidia Taifa kuendelea kusonga mbele kimaendeleo.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Saimon Mayeka, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuleta maendeleo katika Wilaya ya Kongwa. Amesema hapo awali wilaya hiyo ilikuwa na vituo vinne vya afya, lakini kwa sasa vimeongezeka na kufikia saba, hali ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya mama na watoto.

Katika kilele cha maadhimisho hayo, watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii walishiriki kikamilifu, wakiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bi. Shani J. Kamala, pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Utawala, Bi. Violeth Mlinga.







 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI