Polisi wanasema nyumba ya nyota wa muziki wa pop, Rihanna huko Beverly Hills imeshambuliwa kwa risasi.
Maafisa kutoka Idara ya Polisi ya Los Angeles walijibu ripoti za milio ya risasi saa 13:15 saa za eneo hilo (21:15 GMT) siku ya Jumapili. Mshukiwa alipatikana na kukamatwa.
Afisa wa polisi alimwambia mshirika wa BBC nchini Marekani, CBS News, kwamba nyumba iliyolengwa ilikuwa ya Rihanna na kwamba maganda ya risasi yalipatikana katika eneo la tukio.
Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo. Rihanna alikuwa katika jumba hilo la kifahari wakati huo, chanzo cha afisa wa usalama kiliambia Los Angeles Times.
Polisi wanasema mshukiwa, mwanamke mwenye umri wa miaka 30, alisimamisha gari nje ya nyumba hiyo na kufyatua risasi saba kabla ya kuondoka kwa kasi.
Gari lake lilipatikana umbali wa maili nane (kilomita 12) kutoka nyumbani kwa mwimbaji huyo, ambapo mwanamke huyo alikamatwa. Bado hajatambuliwa hadharani.
Septemba mwaka jana, nyota huyo alijifungua mtoto wake wa tatu, msichana, na mpenzi wake A$AP Rocky.
Wawili hao, ambao pia wana watoto wawili wa kiume Riot na RZA, walitangaza ujauzito wa hivi karibuni wa Rihanna katika tamasha la Met Gala mwaka jana.





0 Comments