Header Ads Widget

PROF. KABUDI AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA 26 WA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JUMUIYA YA MADOLA




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Palamagamba J. Kabudi, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola (CFAMM) uliofanyika Machi 8, 2026 jijini London, Uingereza akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.).

Akichangia mjadala, Prof. Kabudi amesema Jumuiya ya Madola inapaswa kubaki kuwa jukwaa muhimu la kushughulikia changamoto za maendeleo na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa (multilateralism) katika kipindi cha sasa chenye changamoto za kisiasa, kiuchumi na kimazingira.

Katika masuala ya uchumi, Prof. Kabudi amesisitiza umuhimu wa kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya nchi wanachama kwa kujifunza kutoka mifano ya ushirikiano wa kikanda kama Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA). Amesema jukwaa la biashara na uwekezaji la Jumuiya ya Madola litasaidia kupunguza vikwazo vya biashara na kuongeza biashara kati ya nchi wanachama.

Vilevile amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika madini muhimu na kuimarisha miundombinu ya kidijitali ili kuhamasisha uwekezaji, uhamishaji wa teknolojia na matumizi ya huduma za serikali mtandaoni. Hatua hizo, amesema zitasaidia kupunguza pengo la kidijitali na kuongeza fursa za kiuchumi kwa vijana.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Ayorkor Botchwey, amewaimiza nchi wanachama kuimarisha ushirikiano kukabiliana na mabadiliko ya mazingira ya kimataifa. Amesema mkutano huo ni fursa ya kujadili mikakati ya kukuza biashara, uwekezaji na kukabiliana na changamoto kama mabadiliko ya tabianchi na changamoto za kiuchumi.

Mkutano wa CFAMM unawakutanisha Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi 56 za Jumuiya ya Madola ikiwa ni jukwaa muhimu la kujadiliana masuala ya kimataifa yanayoathiri maendeleo ya nchi wanachama.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI