Header Ads Widget

*MAKAMU WA RAIS AMWAKILISHA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE.DKT SAMIA SULUHU HASSAN KATIKA MKUTANO WA JUMUIYA YA NCHI ZA AFRIKA, KARIBIANI NA PASIFIKI (OACPS)*


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Sipopo kilichopo Jijini Malabo nchini Guinea ya Ikweta.
 
Katika ufunguzi wa Mkutano huo, salamu za Viongozi mbalimbali zimesisitiza umuhimu wa hitaji la kufanya mageuzi ya Kitaasisi na kimfumo kuwezesha Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) kukabiliana na changamoto zinazoikabili Dunia kwa sasa ikiwemo, migogoro ya kisiasa, vita pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
 
Vilevile, Ufunguzi wa Mkutano huo, umeweka mkazo kwa nchi wanachama kutoa michango kwa wakati ili kuifanya Taasisi ya OACPS kujitegemea kifedha na kuwa sauti huru kwenye jumuiya ya kimataifa. Pia msisitizo umewekwa katika kutumia vema rasilimali watu ambao ni bilioni 1.5 waliopo katika jumuiya hiyo kwa kuwajengea uwezo, ubunifu na matumizi ya akili unde ili kuleta maendeleo.
 
Halikadhalika, Mkutano huo umesisitiza umuhimu wa kukuza biashara baina ya nchi wanachama pamoja na jumuiya zingine za kikanda. Pia kuwajengea uwezo vijana na wanawake ili waweze kushiriki vema katika shughuli za maendeleo.
 
Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huo ni mwendelezo wa jitihada za kuendelea kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kikanda na kimataifa, na kudhihirisha mchango wa nchi katika mijadala ya maendeleo na ushirikiano wa kimataifa.
 
Katika Mkutano huo, Rais wa Angola, Mhe. Joao Manuel Lourenzo, amekabidhi Uenyekiti wa Jumuiya ya OACPS kwa Rais wa Guinea ya Ikweta Mhe. Teodoro Obiang Nguema Mbasogo.
 
Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) yenye jumla ya nchi wanachama 79, ilianzishwa miaka ya 1970 kwa lengo la kuzisaidia kiuchumi na kisiasa nchi zilizopo Afrika, Karibiani na Pasifiki zilizotawaliwa na nchi za Bara la Ulaya. Msingi rasmi wa kisheria wa jumuiya hii uliwekwa tarehe 6 Juni 1975 kupitia Mkataba wa Georgetown. Katika kipindi cha miongo minne, kundi hilo lilijulikana kama Kundi la ACP lakini mnamo Aprili 2020, kufuatia marekebisho ya Mkataba wa Georgetown, kundi hilo lilibadilishwa rasmi kuwa Jumuiya ya Kimataifa ya OACPS.
 
Kauli mbiu ya Mkutano huo ni "OACPS Iliyobadilika na Iliyohuishwa kwa ajili ya Ushirikiano wa Kimataifa Jumuishi, Endelevu na Wenye Kuaminika” (A transformed and renewed OACPS at the service of an inclusive, sustainable and trust-based multilateralism,)". Kauli mbiu hiyo inalenga mabadiliko makubwa ya kimkakati, ambapo OACPS inajipambanua kuwa Jumuiya imara yenye mwelekeo wa kujitegemea.

Katika Mkutano huo, Makamu wa Rais ameambatana na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Suleiman Masoud Makame, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. James Milya, Balozi wa Tanzania Guinea ya Ikweta mwenye makazi yake Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo Mhe. Said Juma Mshana pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Umoja wa Ulaya Mhe. Jestas Nyamanga.
 
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
29 Machi 2026
Malabo – Guinea ya Ikweta.





 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI