Header Ads Widget

LINDI MWAMBAO YAGAWA PIKIPIKI 32 KUIMARISHA HUDUMA KWA WAKULIMA



NA Hadija Omary 


Lindi: Katika juhudi za kuimarisha utendaji kazi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS), Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao kimetoa pikipiki 32 zenye thamani ya shilingi milioni 112 kwa vyama hivyo, kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma kwa wakulima katika maeneo yao.

Makabidhiano hayo yamefanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa chama hicho kwa mwaka 2025/2026, uliofanyika katika makao makuu ya chama hicho, Manispaa ya Lindi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao, Nurdin Said Swalla, amesema kuwa pikipiki hizo zinalenga kutatua changamoto ya usafiri kwa viongozi wa vyama vya msingi, hali itakayowawezesha kuwafikia wakulima kwa urahisi na ufanisi zaidi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho, Ismail Nalinga, amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha vyama vyote 61 vilivyo chini ya usimamizi wa chama hicho vinapatiwa vitendea kazi muhimu. Ameongeza kuwa ugawaji huo utafanyika kwa awamu mbili hadi kukamilika kwake.

Awali, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, alipongeza juhudi zinazofanywa na chama hicho katika kukuza uchumi wa wakulima. Aidha, aliwataka viongozi wa vyama vya msingi kuiga mfano huo kwa kuendelea kubuni na kutekeleza mikakati ya maendeleo.

Baadhi ya wajumbe wa bodi za vyama vya ushirika walioshiriki mkutano huo walieleza shukrani zao kwa kupatiwa pikipiki hizo, wakisema kuwa zitasaidia kupunguza changamoto ya kuwafikia wanachama na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI