Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media
Simanzi na sintofahamu vimetawala katika sakata linalomhusu Jessica Maarufu kwa jina la Mama Nelisa na aliyekuwa mwenza wake, Simon Bryson Mnyola, kufuatia kifo cha mtoto wao, Nilsa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, baada ya kumpoteza mtoto wao, Jessica amejitokeza wazi kumtaka Simon kuacha kile anachodai ni kuendelea “kumtumia” mtoto huyo marehemu kwa manufaa binafsi.
Akizungumza kwa huzuni lakini kwa msimamo, Jessica alieleza kuwa kifo cha mtoto wao kilipaswa kuwa kipindi cha heshima, maombolezo na faragha siyo chanzo cha kujinufaisha au kuvutia huruma ya watu kwa maslahi binafsi.
“Huu ni msiba wangu, ni maumivu yangu naomba aache kulitumia jina la mwanangu kwa mambo ambayo hayana heshima kwa kumbukumbu yake,” alinukuliwa akisema kwa sauti ya majonzi.
Taarifa zinaeleza kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu wanaodai kuwa Simon amekuwa akilitaja jina la mtoto huyo katika mazingira yenye utata, jambo lililozua hisia kali kutoka kwa familia na marafiki wa karibu.
Juhudi za kumpata Simon ili azungumzie tuhuma hizo bado zinaendelea, huku watu wake wa karibu wakidai kuwa yeye pia anapitia kipindi kigumu cha maombolezo.
Wataalamu wa masuala ya kijamii wanasisitiza kuwa katika nyakati za majonzi, ni muhimu kwa wahusika wote kuonyesha heshima, kujizuia na kuepuka vitendo vinavyoweza kuongeza maumivu kwa upande mwingine.
Hata hivyo MATUKIO DAIMA MEDIA kimeendelea kufuatilia kwa karibu tukio hili, huku wengi wakitoa wito wa busara, heshima kwa marehemu, na kulinda utu wa familia iliyo katika kipindi kigumu cha maombolezo.
Hatua zitakazofuata bado hazijafahamika, lakini wazi kuwa suala hili limegusa hisia za wengi na kufungua mjadala mpana kuhusu maadili katika nyakati za maombolezo.






0 Comments