![]() |
| CEO wa Good Deeds Day, Kaynan Rabino (wa pili kulia waliokaa) akiwa katika Picha ya a pamoja katikati tukio hilo |
Dar es Salaam.
WADAU wa Maendeleo na Taasisi mbali mbali wamekutana Jijini Dar es Salaam katika kongamano maalum lililoandaliwa na Good Deeds Day Tanzania, likiwa na lengo la kuwajengea uwezo na kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa matendo mema katika kusaidia jamii.
Good Deeds Day ukiwa ni mwamvuli wa harakati za kujitolea zinazolenga kuchangia maendeleo endelevu kwa kuzingatia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Umoja wa Mataifa, ikiwemo uhifadhi wa mazingira, ustawi wa jamii, usawa wa kijinsia, afya bora, elimu na kupunguza umaskini, kwa lengo la kuleta matokeo chanya na kuboresha maisha ya watu kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kiongozi wa Good Deeds Day Tanzania, Bi. Doroth Namuhisa, amesema kongamano hilo limewakutanisha washiriki 50 kutoka taasisi mbali mbali, likilenga kutoa muongozo, motisha na maarifa juu ya utekelezaji wa matendo mema katika jamii.
“Leo tumekutana hapa Dar es Salaam na tumeshirikisha washiriki 50 kutoka taasisi mbalimbali. Lengo ni kuwaelekeza, kuwapa moyo na kuwajengea uwezo katika masuala ya matendo mema,” amesema Doroth Namuhisa.
Ameongeza kuwa kongamano hilo halijajikita tu katika kujitolea, bali pia limeangazia namna ya kuwezesha jamii kiuchumi na kijamii, sambamba na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mbinu bora za kusaidia jamii zinazowazunguka.
“Hatuzungumzii tu kujitolea, bali pia tunaangalia namna ya kuiwezesha jamii na kushirikiana kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali za maendeleo,” ameongeza.
Aidha, Bi Doroth Namuhisa amesisitiza kuwa kufanya matendo mema kuna mchango mkubwa katika kuboresha afya ya akili, akieleza kuwa ni mojawapo ya matendo mema ambayo mtu anaweza kujifanyia binafsi.
“Matendo mema huleta faraja, amani na furaha. Unapotoa, unajisikia furaha zaidi, jambo ambalo husaidia kutuliza na kuboresha afya ya akili,” amesema.
![]() |
| Kiongozi wa Good Deeds Day Tanzania, Bi. Doroth Namuhisa |
Kwa mwaka 2026, harakati za Good Deeds Day zinaongozwa na kauli mbiu “Tuungane pamoja katika kufanya matendo mema”, sambamba na maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa harakati hizo duniani, zikiwa na kauli mbiu pana zaidi ya “Tuungane kwa pamoja katika kufanya matendo mema kutoka moyoni.”
Amefafanua kuwa msisitizo wa “kutoka moyoni” unalenga kuhimiza watu kufanya matendo mema kwa hiari, bila kulazimishwa, kwa kutumia muda wao, ujuzi na maarifa waliyonayo.
“Tunasisitiza fikiri wema. Ukifikiria mema, utazungumza mema na hatimaye utatenda mema. Dunia inaweza kuwa mahali salama zaidi endapo kila mmoja atachukua jukumu hilo,” amesema.
Kwa mujibu wa muasisi wa Good Deeds Day Tanzania , Doroth Namuhisa, anasema hizi ni harakati za kimataifa zinazohusisha takribani watu milioni 4.5 katika nchi 115, ambapo kila nchi kuanzia mtu binafsi, taasisi, serikali hadi mashirika wanahimizwa kushiriki kufanya matendo mema kila siku.
Ameeleza kuwa kilele cha maadhimisho ya Good Deeds Day hufanyika kila mwaka tarehe 12 Aprili, siku inayotumika kutambua, kupongeza na kusherehekea jitihada za watu na taasisi zinazojitolea kuboresha maisha ya jamii.
Good Deeds Day ni harakati za kujitolea zinazolenga kuchangia malengo ya maendeleo endelevu, ikiwemo uhifadhi wa mazingira, ustawi wa jamii na kuleta matokeo chanya yanayoboresha maisha ya watu kwa ujumla.









0 Comments