NA MATUKIO DAIMA MEDIA.
DAR ES SALAAM.Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kuwa chanzo kikuu cha kero ya foleni katika jiji hilo ni kuruhusu kila aina ya chombo cha usafiri kuingia katika barabara kuu bila mpangilio maalum.
Chalamila ameeleza kuwa hali hiyo imechangia kupungua kwa hadhi na thamani ya jiji, huku ikisababisha msongamano mkubwa wa magari unaochelewesha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa jiji hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini humo Chalamila amesema ili kulirejesha jiji katika muonekano wa kisasa na wenye hadhi, kuna umuhimu wa kuweka utaratibu mpya wa matumizi ya barabara, ikiwa ni pamoja na kupanga upya vyombo vya usafiri vinavyoruhusiwa kutumia barabara kuu.
“Shida ya Dar es Salaam ni kwamba tumeruhusu kila aina ya magari yawe katika barabara kuu hata ambayo hayastahili leo tupo namba E lakini kuna mpaka namba A zipo kwenye barabara kuu ukienda kwenye nchi za wenzetu kama gari yako siyo mpya kwa namba zake zile haiwezi kabisa kuingia mjini huwezi kuikuta kwasababu ikitokea imezima katika hilo ni jambo jingine kabisa.”
Aidha katika hatua nyingine Chamila amesema kuwa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga hawajafukuzwa kabisa katika maeneo yao bali kinachosisitizwa ni kutofanya biashara katika maeneo yanayozuia matumizi rasmi ya barabara.
Ameongeza kuwa kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara kupanga bidhaa zao katika barabara za umma, hali inayosababisha msongamano na usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara, wakiwemo watembea kwa miguu, wasukuma mikokoteni, bodaboda na waendesha magari.
“Sisi hatufukuzi machinga mahali popote, ila wasifanyie biashara barabarani. Jambo hili limefanyika Temeke, ambapo walikuwa wanapanga biashara zao barabarani; sasa magari (mabasi) na watu haviwezi kupita kwenye njia moja kwa wakati mmoja,”
Aidha, amewataka wote waliovamia au kupanga biashara katika barabara za umma kuondoa mara moja vizuizi hivyo na kufuata taratibu zilizowekwa. Amesisitiza kuwa serikali ya mkoa itaendelea kusimamia utekelezaji wa agizo hilo kwa umakini, kwa lengo la kulinda taswira na hadhi ya jiji pamoja na kupunguza usumbufu kwa watumiaji wa barabara
MWISHO.





0 Comments