Na Moses Ng'wat, Mbozi.
VIJANA mkoani Songwe wamehimizwa kuendelea kuilinda na kuidumisha amani ya nchi, wakielezwa kuwa mazingira ya amani ndiyo msingi wa maendeleo na yanawezesha utekelezaji wa miradi inayozalisha ajira na kupanua fursa za kiuchumi kwa vijana.
Wito huo ulitolewa Juni 28, 2026 na Ofisa Mwandamizi wa Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Nasibu Mwaifunga, wakati akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa amani na nguzo zake katika warsha ya siku mbili ya mradi wa Dumisha Amani iliyofanyika wilayani Mbozi.
Warsha hiyo iliwashirikisha vijana 30 kutoka makundi mbalimbali, wakiwemo waendesha bodaboda na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa ufadhili wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Amani na Maendeleo (UNPDF) kupitia Mfuko Mdogo wa Amani na Usalama wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Mwaifunga alisema nguzo ya ulinzi wa vijana inalenga kuhakikisha haki zao zinalindwa, wanashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na wanajiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi.
Aidha, aliwahimiza vijana kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na Serikali ili kujikwamua kiuchumi, akieleza kuwa marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma yanatoa nafasi kwa makundi maalumu, yakiwemo vijana, kunufaika na asilimia 30 ya zabuni za taasisi za umma.
Alisema vijana wenye sifa wanapaswa kujitokeza kuomba zabuni hizo, na endapo watanyimwa haki licha ya kukidhi vigezo, wanapaswa kutumia taratibu za kisheria kudai haki zao.
Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Songwe, Menard Dimoso, alisema katika miezi ya Mei na Juni mkoa huo umefanya makongamano katika halmashauri zote kwa lengo la kuwafikia vijana na makundi maalumu kuhusu fursa za kiuchumi, ujasiriamali na uzalendo.
Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo, Tedy Mwilenga, ambaye ni dereva wa bodaboda, alisema mafunzo hayo yamemjengea uelewa mkubwa kuhusu wajibu wa vijana katika kulinda amani na usalama wa nchi, hivyo ameahidi kuwa balozi wa kuelimisha vijana wengine.
Naye Faraja Nyenza, mfanyabiashara katika Soko la Vwawa, alisema kabla ya kushiriki warsha hiyo hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu fursa zinazotolewa na Serikali kwa vijana, akibainisha kuwa ukosefu wa elimu huchangia migogoro na kuvuruga amani katika jamii.
Alisema elimu waliyoipata itawasaidia vijana wengi kutambua wajibu wao wa kulinda amani huku wakitumia kikamilifu fursa za maendeleo na uwezeshaji wa kiuchumi zinazotolewa na Serikali kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Mwisho.

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)




0 Comments