Header Ads Widget

MBUNGE KASHAKARI ALILIA DARAJA MTO MALAGARASI

 


Na Fadhili Abdallah,Kigoma


MBUNGE wa jimbo la Kigoma Kusini mkoani Kigoma Nuru Kashakari ameitaka serikali kusimamisha miradi yote ya wananchi kwenye jimbo hilo na fedha za miradi hiyo zipelekwe kutekeleza mradi wa ujenzi wa daraja la Malagarasi katika kijiji cha Ilagala wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma kwani kutokuwepo kwa daraja hilo  kumekuwa chanzo kikubwa cha vifo vya mama wajawazito na watoto.


Akizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara cha mkoa Kigoma Kashakari alisema kuwa imechukua miaka 20 sasa mradi huo ukifanyiwa upembezi yakinifu na hakuna matumaini yeyote ya kutekelezwa kwa mradi huo kwa siku za karibuni na kwamba kutokuwepo kwa daraja hilo kunakwamisha uchumi na maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo.



Kauli ya mbunge huyo inafuatia maelezo yaliyotolewa na Kaimu Meneja wa Wakala wa barabara mkoa Kigoma,Mhandisi Chora Kimata aliyeeleza kuwa kwa sasa hakuna fedha za utekelezaji wa mradi huo kwani maombi yaliyopelekwa Benki ya dunia ilionyesha kuwa ilikuwa inaombwa fedha ya  matengenezo ya dharula wakati huo ni mradi mpya huo hivyo haukuwa na vigezo vya kupata fedha.


Mbunge huyo wa jimbo la Kigoma Kusini alisema kuwa Mwambao wa Kusini wa ziwa Tanganyika ni eneo muhimu kwa jimbo na wilaya hiyo kwenye shughuli za kiuchumi na biashara likikusanya asilimia 90 ya mapato ya halmashauri hivyo kutowepo kwa daraja kuna athiri shughuli hizo kwa kiasi kikubwa ikiwemo kudumaza utalii kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mahale.


Akichangia kuhusu changamoto hiyo Mkuu wa wilaya Uvinza, Dinnah Mathaman alisema kuwa wakati wa ziara yake kwenye kampeni ya uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka Raisi Samia aliahidi kuipatia fedha barabara hiyo ili ujenzi wake uanze haraka na mwamba anashangazwa kusikia hata kwenye bajeti yam waka wa fedha barabara hiyo haipo.


Kwa upande wake Mkuu wa mkoa Kigoma,Balozi Simon Sirro ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho alisema kuwa ametembelea na kuona changamoto kubwa ya barabara eneo hilo na athari ya kutokuwepo kwa daraja hilo hivyo akaiomba TANROAADS kuandika maandiko ambayo yanawezesha kupatikana fedha za utekelezaji.



Akitoa hitimisho la changamoto hiyo Meneja wa TANROADS mkoa Kigoma, Mhandisi Chora Kimata alisema kuwa upembuzi yakinifu ya mradi huo umeshafanyika na kwamba watawasiliana na wizara ya ujenzi kuona barabara hiyo inapatiwa fedha ili ianze kujengwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI