Header Ads Widget

TFS, JESHI LA POLISI WAIMARISHA OPERESHENI KUDHIBITI MAGENDO YA MAZAO YA MISITI MAJINI


Mwanza, Februari 16, 2026 — Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeahidi kuimarisha ushirikiano wake na Jeshi la Polisi Tanzania katika kukabiliana na usafirishaji haramu wa mazao ya misitu kupitia maziwa na bahari, hususan mikoko kutoka maeneo ya pwani.

Ahadi hiyo imetolewa na Kamanda wa TFS Kanda ya Ziwa, SACC Ebrantino Mgiye, wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya siku 14 kwa maofisa 11 wa TFS yaliyofanyika katika Chuo cha Polisi Wana Maji Mwanza.

Kwa mujibu wa Mgiye, mafunzo hayo yanalenga kuongeza ufanisi wa doria na oparesheni maalum za kuwabaini na kuwakamata wahalifu wanaotumia njia za maji kusafirisha mazao ya misitu kinyume cha sheria.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha ulinzi wa rasilimali za taifa na kukomesha vitendo vya uhalifu vinavyoendelea katika maeneo ya maji.


“Ushirikiano wetu na Jeshi la Polisi utaongeza nguvu katika operesheni za pamoja na kuhakikisha rasilimali za misitu zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Mgiye.

Akifunga rasmi mafunzo hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilibroad Mutafungwa, alisema Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na taasisi za serikali katika kulinda rasilimali za taifa.

Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya uhalifu majini yanahitaji wataalamu waliopata mafunzo ya vitendo na wenye utayari wa kimwili na kiakili.


Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Polisi Wana Maji Mwanza, SACP Ndagile Makubi, alisema chuo hicho kitaendelea kutoa mafunzo ya kitaalamu ili kujenga uwezo wa maofisa katika kudhibiti uhalifu majini na kuimarisha operesheni shirikishi.

Baadhi ya maofisa waliohitimu mafunzo hayo walisema wako tayari kutumia ujuzi walioupata, ikiwemo mbinu za uokozi, matengenezo ya boti za doria na mbinu za kukabiliana na wahalifu majini, ili kuimarisha ulinzi wa rasilimali za misitu nchini.








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI