Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
Wakati dunia ikiendelea kupaza sauti kuhusu umuhimu wa kinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na magonjwa ya zinaa, takwimu zinaonesha kuwa matumizi ya kondomu nchini yameshuka kwa takribani asilimia tano.
Hii si namba ya kupuuzwa ni ishara inayopaswa kuamsha mjadala mpana na hatua za haraka katika kulinda afya ya jamii.
Kupungua huku kunakuja licha ya kampeni za muda mrefu za uhamasishaji na upatikanaji wa kondomu katika vituo vya afya na maeneo mbalimbali ya umma.
Je, tatizo ni nini? Je, ni uchovu wa kampeni, kuongezeka kwa dhana potofu, au kupungua kwa hofu ya maambukizi kutokana na maendeleo ya tiba?
Baadhi ya wananchi wa Dodoma wanasema bado kuna pengo la elimu sahihi kuhusu matumizi ya kondomu.
Ingawa asilimia hiyo inaweza kuonekana ndogo kwa mtazamo wa haraka, kwa tathmini ya afya ya umma ni takwimu yenye uzito mkubwa.
Kupungua huku kunamaanisha kuwa watu zaidi wako katika hatari ya kuambukizwa au kupata mimba zisizotarajiwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Takwimu hizi zinajitokeza wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha World Condom Day, siku inayolenga kuhamasisha matumizi sahihi ya kondomu kama njia muhimu ya kinga.
Maadhimisho haya yanalenga kukumbusha jamii kuwa licha ya maendeleo ya tiba, kinga bado ndiyo silaha madhubuti zaidi katika kupunguza maambukizi mapya.
Selina Kusena amesema kuwa changamoto si upatikanaji pekee, bali ni uelewa wa vitendo.
Wapo wanaochelewa kuvaa kondomu hadi baada ya kuanza kujamiiana, wengine huzitumia zaidi ya mara moja au kuzihifadhi katika mazingira yasiyo salama kama mifukoni kwa muda mrefu, jambo linaloweza kuathiri ubora wake.
"Matumizi ya namna hii hupunguza ufanisi wa kondomu na kuongeza hatari badala ya kupunguza, " Amesema Selina
Laizer Mollel amesema imani potofu zimeendelea kuwa kikwazo kikubwa Dhana kwamba matumizi ya kondomu hupunguza raha au kuashiria kutokuaminiana katika mahusiano imejengeka kwa baadhi ya watu.
Amesema Vijana, ambao ndio kundi lililo katika hatari zaidi kutokana na mabadiliko ya kitabia na shinikizo la rika, wameonekana kuathirika zaidi na mitazamo hii.
Aidha, unyanyapaa unaohusishwa na kuchukua au kununua kondomu hadharani umewafanya baadhi ya watu kukosa ujasiri wa kuzitafuta.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NASHCoP), Boniface Silvani, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuimarisha juhudi za utoaji elimu ya kinga kwa makundi mbalimbali, hususan vijana.
Ameeleza kuwa pamoja na kuhimiza matumizi ya kondomu, serikali inasisitiza maadili mema na kujiepusha na ngono katika umri mdogo kama sehemu ya mkakati mpana wa kupunguza maambukizi mapya.
Kwa mujibu wa Dk. Silvani, elimu inayotolewa inalenga kubadili mitazamo na kuongeza uelewa wa kina kuhusu namna sahihi ya kutumia kondomu.
Amesema kuwa bila elimu sahihi, hata kama kondomu zitapatikana kwa wingi, hazitaweza kufikia lengo lililokusudiwa la kupunguza maambukizi.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Kinga kutoka Wizara ya Afya Tanzania, Zeye Nkomela, amesema serikali imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya bila vikwazo.
Mikakati hiyo ni pamoja na usambazaji wa kondomu bure katika vituo vya afya, zahanati na hospitali, pamoja na kampeni za uelimishaji kupitia mikutano ya hadhara, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi wote, mijini na vijijini, ili waweze kufanya maamuzi sahihi yanayohusu afya zao.
Pia amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kupanua wigo wa elimu na huduma.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa sababu nyingine inayochangia kushuka kwa matumizi ya kondomu ni kupungua kwa hofu ya maambukizi kutokana na upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs).
Baadhi ya watu wameanza kuamini kuwa kutokana na uwepo wa dawa hizo, hatari ya maambukizi imepungua au UKIMWI una tiba kamili.
Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa ARVs husaidia kuboresha afya ya mtu aliyeambukizwa lakini hazizuii maambukizi mapya kwa mtu ambaye hajachukua tahadhari.
"Hali hii inaonesha kuwa mapambano dhidi ya UKIMWI yanahitaji mkakati jumuishi unaogusa nyanja zote za jamii, " Amesema Nkomela .
Hata hivyo amesema Elimu inapaswa kuanzia ngazi ya familia, ambapo wazazi wanahimizwa kuzungumza kwa uwazi na watoto wao kuhusu afya ya uzazi kwa kuzingatia umri wao.
" Kuna haja sasa Shuleni, mitaala inapaswa kuendelea kujumuisha masuala ya afya ya uzazi kwa njia inayofaa na inayozingatia maadili ya jamii, " Amesema n.
Viongozi wa dini, taasisi za kiraia na wanaharakati wa afya wana nafasi muhimu katika kuondoa unyanyapaa na kuhimiza mazungumzo ya wazi kuhusu ngono salama.
Kadri jamii inavyokuwa tayari kujadili masuala haya bila hofu au aibu, ndivyo inavyokuwa rahisi kubadili mitazamo na kuongeza matumizi sahihi ya kondomu.
Kwa ujumla, kushuka kwa matumizi ya kondomu kwa asilimia tano ni kengele ya tahadhari.
Ni ujumbe unaoashiria kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza maambukizi kwa miaka iliyopita, bado kuna changamoto zinazohitaji nguvu mpya.
Maadhimisho ya Siku ya Kondomu Duniani yanapaswa kuwa zaidi ya tukio la kalenda; yawe chachu ya kuchochea hatua za vitendo.
Iwapo elimu itaongezwa, unyanyapaa utaondolewa na huduma kuendelea kuboreshwa, inawezekana kurejesha mwelekeo chanya wa matumizi ya kondomu.
Hatua hizo zitachangia si tu kupunguza maambukizi mapya, bali pia kulinda afya ya kizazi cha sasa na kijacho Mapambano haya yanahitaji mshikamano wa wote,serikali, jamii na kila mmoja binafsi,kwa sababu afya ya taifa ni jukumu la pamoja.












0 Comments