Halmashauri ya manispaa ya Bukoba mkoani Kagera imepitisha ya bajeti ya zaidi shilingi billioni 40.7 Kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo sekta ya Afya na Elimu Kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Akizungumza wakati akiwasilisha rasmi ya bajeti hiyo katika kikao cha baraza la madiwani cha kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka wa fedha, Afsa mipango wa manispaa ya Bukoba Melkion Komba amesema kuwa fedha hiyo itatokana na mapato ya ndani, wahisania na fedha kutoka serikali kuu.
Aidha Komba amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 wanatarajia kumalizia miradi viporo, ujenzi wa hospitali ya wilaya, ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na ununuzi wa madawati katika shule mbalimbali katika manispaa ya Bukoba.
"kipaumbele chetu katika mwaka wa huo wa fedha mapato yetu ya ndani pamoja fedha kutoka kuu utailekeza katika sekta ya Elimu kununua thamani kwa maana ya madawati kutokana na watoto kukaa chini".
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Rwamishenye Sued Kagasheki ametaka katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ujikite kwanza katika miradi viporo ambayo ilisalia katika mwaka wa fedha 2025/2026, na pia ametaka kuzingatiwa kwa suala la usafi wa mazingira.
"naomba tusikimbilie utekelezaji wa miradi mipya wakati kuna miradi ya viporo, ofisi hii inatakiwa kuwa kama inavyoonekana ndani, lakini na mkandarasi anayeshughulikia taka alipwe fedha yake Kwa wakati maana bajeti yake imewekwa".
Naye Diwani wa kata ya Kashai Ramadhan Kambuga ametaka usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa bajeti hiyo ili kutoa matokeo chanya, kwani fedha ya mapato ya ndani na kutoka serikali kuu ni kodi ya wananchi hivyo miradi ya itakayotekelezwa iendane na thamani halisi ya fedha.
"mheshimiwa Naibu Meya upitishwaji wa bajeti ni jambo moja na utekelezaji wa bajeti hiyo ni jambo lingine, tunahitaji usimamizi wa utekelezaji kwani fedha ya mapato ya ndani na kutoka serikali kuu ni kodi ya watanzania, na miradi iendane na thamani halisi ya fedha".
Katika hatua nyingine Halmashauri ya manispaa ya Bukoba imepanga kukusanya mapato ya shilingi billioni 4.8 ili kuwezesha utekelezaji wa bajeti hiyo.
Bajeti ya mwaka wa fedha ujao kwa manispaa ya Bukoba inaongezeko ya zaidi ya shilingi billioni 2 kutoka shilingi billioni 38.92 kwa mwaka huu wa fedha 2025/2026.









0 Comments