Header Ads Widget

MRADI WA SEQUIP-AEP WAWAREJESHA WANAFUNZI 13,000 WALIOKATISHA MASOMO YA SEKONDARI

 

Na Lilian Kasenene,Morogoro

Matukio DaimaApp 


WANAFUNZI 13,000 wenye umri kati ya miaka 13 na 21 waliokatisha masomo ya sekondari kwa sababu mbalimbali ukiwemo ujauzito wamejisajili na kurudi upya kuendelea na masomo kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala (SEQUIP- AEP).


Mradi huo ulianza kutekelezwa  mwaka 2022 hadi kufikia mwaka huu (2026).


Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Profesa Philipo Sanga alisema hayo mjini Morogoro alipofungua kikao kazi cha siku nne cha kutathimini utekelezaji wa kazi za mradi wa SEQUIP- AEP kilichowashirikisha watekelezaji wa mikoa 26 ya Tanzania Bara.


Profesa Sanga alisema Mradi huo umetekelezwa na taasisi hiyo iliyopo  chini ya Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TEMISEMI) kwa ufadhili wa Benki Dunia.


Alisema kazi ya Taasisi iliyopewana Serikali ni kujishughulisha na kuwarejesha shuleni watoto waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali zikiwemo mimba za utotoni , ajira za watoto , kuolewa kabla ya wakati pamoja na hali za kiuchumi za familia zao .


“Tulipewa jukumu la kuwarejesha hao na katika hilo tulipewa kipimo maalumu ndani ya miaka mitano ya mradi ulipoanza mwaka 2022 na mwaka huu ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa mradi,”alisema Profesa Sanga .


Profesa Sanga alisema katika kipindi hicho ,Taasisi ilipewa jukumu la kurejesha watoto 12,000  na wakati inafanyika tathimini ya utejelezaji wa jukumu lililotolewa na Serikali kumekuwepo mafanikio makubwa.


“Nisema tathimini ya jumla ya kuwarejesha watoto shuleni 12,000 tuliopewa na Serikali  nafurahi kusema tumetimiza na tumezidisha na mpaka hivi sasa tumerejesha watoto zaidi ya 13,000 na tumetekeleza kwa asilimia zinazozidi 100 na haya ni mafanikio makubwa”alisema  Profesa Sanga.


Alisema wanufaika wengine ni kwa wanafunzi kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita, vyuo vya kati na vyuo vikuu, na imeifanya Serikali kuonelea kuna haja ya kufikiria jinsi ya kuifanyaTaasisi iendelee kutekeleza jukumu hilo kwa njia zingine .


 “Watoto hawa wanaendelea kuwepo kila mwaka kwa kushinda kuendelea kwenye mfumo rasmi wa elimu na wanaposhindwa hawawezi kuachwa nyuma,” alisema Profesa Sanga.


Katika hatua nyingine alisema mradi huo pia umewezesha uboreshaji wa miundombinu ya usomaji kwa kujenga majengo ya madarasa katika vituo vilivyopo mikoani, hosteli , maktaba


Profesa Sanga alisema katika kutekeleza mradi huo waligundua kuwa licha ya mafanikio hayo makubwa, zipo changamoto mbalimbali katika jamii wanazotoka hao watoto.


“Jamii hasa wazazi na walezi  wengi walishawakatia  tamaa watoto hao  na wanapoambiwa kuna fursa ya pili ,wazazi na walezi wengi wao whawajakulibali jambo  hilo endapo kuna uwezekano wa kusoma tena,”alisema Profesa Sanga.


Kwa upande wao wakufunzi wakazi wa elimu mikoa kutoka Taasisi hiyo,Kasim Dallu kutoka Iringa, Rainer Chale wa Simiyu pamoja na Meneja wa Kampasi ya Ruvuma , Dk Hellen Lyamuya kwa nyakati tofauti walisema mradi huo umewapa manufaa makubwa  watoto wakike na wakiume waliokatisha masomo na kurejea tena shuleni kwa mfumo usiorasmi wakinufaika vyema na masomo yao.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI