Na Joyce Ndunguru, Arusha
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), ameizindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) leo Januari 9, 2026, jijini Arusha.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Dkt. Kijaji amewapongeza wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA kwa kuteuliwa kwao, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko.
“Kwa namna ya kipekee nikupongeza sana Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko kwa kuendelea kuaminiwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Bodi kwa awamu nyingine tena. Kwa dhati ya moyo wangu, ninawapongeza wote kwa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bodi ya TAWA, hongereni sana”, amesema Waziri Kijaji.
Sambamba na pongezi hizo, Waziri Kijaji ametoa rai kwa Bodi ya TAWA kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika uboreshaji wa miundombinu kwenye maeneo ya hifadhi, kwa lengo la kuyaongezea thamani, kuvutia wawekezaji na kuongeza idadi ya watalii.
“Ninaielekeza Bodi hii ninayoizindua leo kuwaita wawekezaji waje kuwekeza nasi kwenye miundombinu muhimu ili tuweze kunufaika na vivutio hivyo”, amesema Waziri Kijaji.
Aidha, Waziri Kijaji ameisisitiza Bodi ya TAWA kuendelea kuimarisha ulinzi wa maeneo ya hifadhi pamoja na kuongeza bidii katika udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu kwa kutumia teknolojia ya kisasa, kuongeza vituo vya askari, kuboresha vitendea kazi na kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni nane ifikapo mwaka 2030.
Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko, amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteua kwa mara ya pili kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA.
Aidha, Meja Jenerali (Mstaafu) Semfuko amesema kuwa kwa kushirikiana na wajumbe wa Bodi ya TAWA wataendelea kuwa wabunifu na wazalendo katika kuhakikisha TAWA inakuwa kinara katika uhifadhi, utoaji wa huduma bora na kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.
Sambamba na hilo, Semfuko ameahidi kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatatekelezwa ipasavyo, huku Bodi yake ikishirikiana kwa karibu na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau wa kisekta katika kuhakikisha malengo ya TAWA yanafikiwa.
Katika hafla hiyo ya uzinduzi, Waziri Kijaji aliambatana na Naibu Katibu Mkuu – Utalii, Bw. Nkoba Mabula, pamoja na viongozi wengine kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.


















0 Comments