Header Ads Widget

POLISI KAGERA WATOA ONYO KALI KWA WATAKAOVURUGA UCHAGUZI MKUU.

 

KAMANDA wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda akiongea na waandishi wa Habari.


Na Shemsa Mussa -Matukio Daima Bukoba


KAMANDA wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, ametoa onyo kali kwa wananchi watakaokusudia kuleta vurugu au kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani wakati wa zoezi la Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.


Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Bukoba, Kamanda Chatanda alisema zimebaki siku tano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, na kwamba Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.


Alisema kumekuwepo na taarifa zinazoenezwa kwamba baadhi ya wananchi wanapanga kufanya ulinzi wa kura, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu, kwani jukumu hilo ni la Jeshi la Polisi pekee.


“Ulinzi wa kura ni jukumu la Polisi, sio mwananchi. Wale wanaotaka kujichukulia jukumu hilo wajue tupo kazini. Mpiga kura akikamilisha zoezi lake anatakiwa kuondoka eneo la kupigia kura na kurejea nyumbani kwa utulivu ili kudumisha ustaarabu,” alisema Chatanda.


Aidha, Kamanda huyo alionya dhidi ya vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha vurugu au uvunjifu wa amani, akibainisha kuwa uchaguzi ni haki ya kikatiba inayopaswa kutekelezwa kwa kufuata sheria na kanuni za nchi.


Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu yeyote atakayejihusisha na uchochezi, upotoshaji au vitendo vya uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi, na kuwataka wananchi kushiriki zoezi hilo kwa amani huku wakidumisha umoja na mshikamano wa kitaifa.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI