Na Matukio Daima Media
KIONGOZI Mkuu wa Taasisi ya Twariqa Tanzania, Sheikh Said Hamis Migire, amesisitiza umuhimu wa Kila Mtanzania kuwajibika katika kudumisha amani na utulivu kabla, wakati wa upigaji wa kura na hata baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 akifananisha amani na yai ambalo likivunjika ni vigumu kulirejesha katika hali yake ya awali.
Akizungumza na waandishi wa habari pembezoni mwa dua maalumu ya kuombea amani iliyofanyika katika Zawia Kuu, Makao makuu ya taasisi hiyo jijini Arusha, na kuhudhuriwa na mamia ya waumini kutoka maeneo mbalimbali nchini, Sheikh Migire amesema ni muhimu kila Mtanzania kujiepusha na vurugu na viashiria vingine vyovyote vyenye kutishia tunu za Taifa, akihimiza kutafakati kabla ya kuchukua hatua yoyote inayoenda kinyume na tamaduni na ustaarabu.
“Amani ni kama yai likivunjika ni ngumu sana kulirudisha. Tumeona mataifa mengi ya Afrika yaliyopoteza amani, na sasa wanajuta." Amesema.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Twariqa Taifa, Sheikh Haruna Hussen ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini kuungana kwa pamoja katika maombi ya kuombea amani, akisisitiza kuwa jukumu la kulinda amani ni la kila Mtanzania.
“Na sisi kama viongozi wa dini tunao wajibu wa kuhubiri amani usiku na mchana. Amani ni msingi wa taifa.
Tunawaomba Watanzania wasidanganyike bali tushike amani yetu kwa mikono miwili." Amesema Sheikh Haruna.
![]() |








0 Comments