Na. Mwandishi Wetu, Mikumi.
KIKAO kazi cha Maafisa Utalii wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kimefanyika leo tarehe 6 Oktoba, 2025 katika Hifadhi ya Taifa Mikumi, kikiwa na lengo la kujadili mbinu bora za kuboresha huduma za utalii na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Lengo kuu la kikao hicho ni kubadilishana uzoefu, kujenga uelewa wa pamoja, na kujifunza mbinu za kisasa za utangazaji wa vivutio vya utalii ndani ya Hifadhi za Taifa Tanzania, pamoja na kuweka mikakati thabiti ya kuboresha huduma za utalii.
Hii ni katika kipindi ambacho Shirika linaendelea kusisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia, ubunifu, na akili mnemba (artificial intelligence) katika kuboresha huduma kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.
Kikao hicho kimeongozwa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Neema Mollel, ambaye pia ni Mkuu wa Ofisi Kiunganishi Mkoa wa Dar es Salaam. Aidha, kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Shirika hilo akiwemo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Jully Bede Lyimo, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo na Biashara TANAPA kutoka Makao Makuu ya Shirika hilo, pamoja na Makamishna na Maafisa kutoka Ofisi za Kanda za Mashariki, Magharibi, Kusini, na Kaskazini, sambamba na Maafisa Malikale kutoka vituo vitano ikiwemo Isimila, Nyumba Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Makumbusho ya mkwawa, Dr Livingstone na kituo cha makumbusho ya utumwa Caravan serai bagamoyo.
Aidha, kikao hicho kimehusisha watoa mada kutoka nje ya Shirika waliotoa mafunzo maalum kwa Maafisa Utalii kuhusu utoaji wa huduma bora kwa wateja, usimamizi wa maadili ya kazi, na mbinu bora za uhusiano na wateja (customer relations) kwa lengo la kuboresha taswira na ubora wa huduma zinazotolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania.
0 Comments