Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma
TAASISI ya FDH Sports Promotion imezindua rasmi mashindano ya mpira wa miguu yanayojulikana kama “Nishati Safi Cup” katika Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ajenda yake ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Watanzania wote.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, Mratibu wa mashindano kutoka FDH Sports Promotion, Noel Simon, amesema taasisi hiyo imeamua kutumia michezo hususan mpira wa miguu kama nyenzo ya kuwaunganisha watu katika maeneo mbalimbali ya nchi ili wapate elimu ya moja kwa moja kuhusu umuhimu wa kuachana na matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa na kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi kama gesi, umeme na mkaa mbadala.
Amesema kupitia mashindano hayo, FDH inatarajia kuzifikia jamii nyingi zaidi kwa urahisi na kwa njia ya burudani, jambo linalosaidia ujumbe kufika kwa haraka na kueleweka kwa urahisi.
Aidha, amebainisha kuwa taasisi hiyo ina mpango wa kupeleka mashindano hayo katika kila mkoa wa Tanzania ili kuendelea kuchochea uelewa na hamasa kuhusu matumizi ya nishati safi kwa wananchi wa kada mbalimbali.
Noel Simon ameishukuru Kampuni ya Taifa ya Madini Tanzania (STAMICO), ambayo ni mdhamini mkuu wa mashindano hayo, kwa kuendelea kushirikiana na FDH Sports Promotion katika kuhakikisha ajenda ya matumizi ya nishati safi inafanikishwa kwa vitendo.
Amesema kuwa mchango wa STAMICO umewezesha upatikanaji wa mkaa mbadala na ambao hauna madhara ya fya kwa binadamu wala mazingira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi Mama ya Foundation for Disabilities Hope (FDH), Maiko Salali, amesema ni wakati muafaka sasa kwa Watanzania kuachana na matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida, ambao si rafiki kwa afya wala mazingira, na kuanza kutumia nishati safi ambayo ni salama, rafiki wa mazingira na yenye kuokoa muda na rasilimali.
Amesema kuwa matumizi ya nishati safi yanasaidia pia kupunguza tatizo la ukataji miti hovyo, ambalo linachangia kwa kiwango kikubwa mabadiliko ya tabianchi.
Ameongeza kuwa kupitia mashindano haya, jamii itapata elimu ya kutosha kuhusu njia bora na mbadala za upishi salama, huku akitoa pongezi kwa STAMICO kwa kuendelea kuwa bega kwa bega na FDH katika kufanikisha dhamira hiyo na kuwapatia mkaa ambao ni ujulikanao kama rafiki Briquettes unaodumu zaidi , rafikiwa mazingira, rafiki kwa matumizi na rafiki kwa bei .
Ameishukuru pia Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kushirikiana na FDH na kuwa sehemu ya taasisi zinazosaidia kutekeleza ajenda ya nishati safi nchini.
TANAPA ikiwa ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, yenye jukumu la kusimamia hifadhi za taifa, imekuwa mstari wa mbele katika kulinda mazingira na kuhimiza matumizi ya nishati safi ili kupunguza uharibifu wa misitu na makazi ya wanyamapori.
Vilevile, TAWA ambayo ni mamlaka ya usimamizi wa maeneo ya wanyamapori nje ya hifadhi za taifa, imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa jamii juu ya ulinzi wa mazingira na umuhimu wa nishati mbadala kama njia ya kupunguza utegemezi wa misitu kwa kuni na mkaa.
Mashindano ya Nishati Safi Cup yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko ya tabia na mitazamo ya jamii kuhusu matumizi ya nishati ya kupikia, huku vijana na wapenzi wa michezo wakihusishwa moja kwa moja katika kampeni hiyo ya kitaifa.
Mwisho
0 Comments