NA MATUKIO DAIMA MEDIA.
BUNDA.Wananchi wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara wameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kwa kuwajengea vizimba vya kuzuia mamba kuwadhuru wakati wa kuchota maji ziwani na kufanya shughuli zingine pembezoni mwa Ziwa Victoria ikiwemo kufua na kuoga.
Wamesema hayo leo Oktoba 6, 2025 kwa nyakati tofauti wakati timu ya wataalam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilipotembelea maeneo ya vizimba hivyo.
Akizungumza katika ziara hiyo,Mkazi wa Mwiseni,kata ya Butimba, Bi. Gabaseki Gervaz amesema wamefurahi sana kupata kizimba kutokana na changamoto walizokuwa wanakutana nazo mwanzoni za kukamatwa na mamba wanapofanya shughuli zao pembezoni mwa ziwa.
"Serikali baada ya kuona tunateseka kutokana na vifo kila mwaka kwa kuuliwa na mamba ikajenga kizimba hiki" amesema Bi. Gervas na kuiomba Serikali kuongeza vizimba vya ziada kwa ajili ya jinsia ya kiume na mifugo.
Naye, Bw. Tabingwa Charles Kasao mkazi wa kitongoji cha Nampangala kata ya Kisorya ,Bunda mkoani Mara ameishukuru Serikali kwa kujali wananchi na kujenga kizimba katika eneo hilo na kuepusha vifo vya wananchi wakiwemo wanafunzi wanaotumia ziwa hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwiseni, Bw. Msiba Chiharata amesema kutokana na faida za vizimba katika kuzuia mamba wanaodhuru wananchi, wameweka adhabu kwa wananchi wanaojaribu kuharibu eneo la Kizimba.
"Tumeweka adhabu kwa mtu yeyote atakayefanya uharibifu wa aina yeyote ile iwe ni kuanika nguo au kuingiza mifugo eneo la vizimba faini ni shilingi laki moja" amesema Bw.Msiba.
0 Comments