Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mgombea ubunge jimbo la Kigoma mjini kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameahidi kukomesha mikopo yenye riba kubwa maarufu kausha damu endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kuanzisha mfuko maalum utakaotoa mikopo bila riba.
Zitto alisema hayo wakati wa kampeni zake za kuwania nafasi hiyo zilizofanyika katika kata ya Kagera manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo alisema kuwa akiwa mbunge ataweka shilingi bilioni moja ili wananchi waweze kukopa.
Mgombea huyo alisema kuwa mikopo yenye riba kubwa imekuwa changamoto kubwa kwa wajasiliamali kwani huwafanya shughuli zao kukua kwa tija lakini pia taratibu zao hazina utu na staha na wakati mwingine kunyang'anywa mali zao kwa kushindwa kurudisha mikopo kwa wakati.
Kabwe alisema kuwa mpango wa utoaji mikopo ni sehemu ya mambo ya kipaumbele atakayoshughulikia ikiwa ni pamoja na kuanzisha mpango wa hifadhi ya jamii ambao ndani yake kutakuwa na taratibu za utoaji mikopo kwa wajasiliamali na huduma za afya kwa ajili ya matiababu kwa wote.
Aidha katika ahadi zake mgombea ubunge huyo wa jimbo la Kigoma Mjini alisema kuwa wakipewa ridhaa ya kushika halmashauri ya manispaa Kigoma Ujiji kwa kuwa na mbunge na idadi kubwa ya madiwani wataligeuza eneo la Kagera Ujiji Manispaa ya Kigoma Ujiji kuwa Satelite City (Mji wa pembeni wenye huduma muhimu za kijamii) hivyo ameomba wananchi wa jimbo hilo kumchagua ili kuweza kutekeleza mipango hiyo.
Kwa upande wake Mgombea udiwani kata ya Kagera Manispaa ya Kigoma Ujiji, Kana Abdallah alisema akichaguliwa kuwa diwani wa kata hiyo jambo la kwanza itakuwa kupigania malipo ya fidia ya wananchi ambao maeneo yao yalichukuliwa na Mpango wa Uwekezaji (KISEZ) lakini malipo imekuwa na vurugu.
0 Comments