Header Ads Widget

SERIKALI YAZINDUA KAMATI ZA USIMAMIZI WA MKAKATI WA MAPATO YA NDANI.

 



Na Hamida Ramadhan, MatukioDaimaMedia Dodoma



SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha imezindua Kamati Tendaji na Kamati ya Wataalam kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Muda wa Kati wa Kuongeza Mapato ya Ndani ambao unalenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kupunguza utegemezi wa misaada ya wahisani


Akizungumza jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa kamati hizo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt Natu El-Maamry Mwamba alisema kuwa mkakati huo utaisaidia Serikali kuwa na bajeti endelevu na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kutumia mapato ya ndani badala ya kutegemea misaada ya nje


Amesema kamati hizo zimeundwa kwa kuzingatia weledi na uzoefu wa wataalamu kutoka serikalini na sekta binafsi ambapo Kamati Tendaji na Kamati ya Wataalam watashirikiana kuhakikisha mkakati unatekelezwa kwa ufanisi na kwa matokeo chanya


Dkt Mwamba ameeleza kuwa mkakati huo umejikita katika maeneo matatu ambayo ni maboresho ya sera za mapato usimamizi wa ukusanyaji wa mapato na maboresho ya sheria lengo kuu likiwa ni kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji


"Katika maeneo ya kodi mkakati unapendekeza kuandaliwa kwa Sera ya Taifa ya Kodi ambayo itatoa mwelekeo wa uboreshaji wa sera za kodi kuboresha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato kuimarisha utii wa hiari wa walipakodi kuboresha usajili wa walipakodi kuimarisha usimamizi wa misamaha ya kodi kuboresha marejesho ya kodi na viwango vya kodi kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kutoka katika uchumi wa kidijitali pamoja na kuboresha usimamizi wa mapato ya forodha, "amesema


Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera Dkt Johnson Nyella amesema kuwa jukumu la kamati hizo ni kuhakikisha Taifa linajenga msingi imara wa ukusanyaji mapato kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kuimarisha uwezo wa kujitegemea kiuchumi


Amesema kamati hizo zitakuwa zikikutana mara kwa mara kufanya tathmini ya utekelezaji wa mkakati huo ambao unatarajiwa kuanza kutekelezwa rasmi katika mwaka wa fedha 2025 2026 lengo likiwa ni kujenga mfumo endelevu wa mapato unaowezesha maendeleo ya Taifa kupitia vyanzo vya ndani


Mwisho. 





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI