Na Mwandishi wetu, Matukio Daima Busega.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu imejipanga kusajili zaidi ya vikundi 100 vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye ulemavu katika Mfumo wa Manunuzi ya Umma NeST hadi ifikapo Juni 2026.
Hayo yamebainishwa na Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Angela Mvaa, na kueleza kwamba hatua hiyo inalenga kuwezesha vikundi vya Wanawanawake, Vijana na Wenyeulemavu kunufaika na asilimia 30 ya thamani ya bajeti ya halmashauri ya ununuzi wa umma kwa mwaka wa fedha kwa ajili ya makundi hayo.
Akifunga mafunzo ya siku mbili ya vikundi vya Wanawake, Vijana na Wenyeulemavu wilayani humo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Musombwa Buliro, ametoa rai kwa washiriki wayatumie kama chachu ya kwenda kusajili vikundi Maalum kwenye Mfumo wa Manunuzi ya Umma (NeST) ili waweze kunufaika na fursa za kiuchumi kupitia zabuni zinazotolewa na taasisi za umma.
Meneja Utafiti na Program Taasisi ya Wajibu, Moses Kimaro na Mkufunzi wa Mafunzo hayo kutoka Mamlaka ya Udhiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Glory Didas, wamewataka washiriki hao kwenda kuwa mbegu kwa wengine kuwajengea uelewa juu ya fursa ya kupata fedha kupitia zabuni za umma badala ya kutegemea mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri pekee.
Ester Juma na Christopher Msiba ni miongoni mwa washiriki wa mfunzo hayo, wanasema yamewahamasisha kwenda kuanzisha na kurasimisha vikundi maalum na kuhakikisha vinashiriki kikamilifu katika mchakato wa manunuzi ya umma kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Washiriki 50 kutoka vikundi vya Wanawake, Vijana na Wenyeulemavu wameshiriki hayo yaliyofanyika kwa ufadhili wa Taasisi ya Wajibu.
Mwisho.
0 Comments