Header Ads Widget

USSI: TUWAPE USHIRIKIANO POLISI KUIMARISHA USALAMA

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Wananchi Mkoani Kigoma wameobwa kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili liweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya ulinzi wa raia na mali zao na kuwezesha utekelezaji wa shughuli za kiuchumi kufanyika kwa Amani na salama.

Wito huo umetolewa na kiongozi  wa mbio za Mwenge wa uhuru mwaka 2025 Ismail Alli Ussi wakati akizindua kituo cha polisi cha Nyamnyusi katika halmashauriya wilaya Kasulu mkoani Kigoma na kubainisha kuwa jeshi la polisi linapaswa kuungwa mkono kuweza kutimiza majukumu yake.

Katika hilo alisema kuwa ni lazima wananchi watoe taarifa katika kufichua mambo ya uhalifu lakini pia kulitumia jeshi la polisi katika migogoro ya shughuli za kijamii sambamba na kuomba ulinzi wanapokuwa na shughuli zao.

Akizungumza na halaiki ya wananchi wa wilaya ya Kasulu waliojitokeza katika uzinduzi huo wa kituo cha polisi kiongozi huyo alisema kuwa bila kuwepo kwa ulinzi wa polisi ni ngumu wananchi kufanya shughuli zao za kijamii, biashara na shughuli za kiuchumi na hilo linathibitishwa na jirani zao ambao kila siku wanakimbilia hapa nchini kuomba hifadhi baada ya kuvurugika kwa hali ya ulinzi na usalama.

Awali Mkuu wa wilaya Kasulu, Isack Mwakisu alisema kuwa mradi huo umejengwa kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri na hiyo inatokana na uhitaji wa halmashauri ambayo imemamliza mradi wake wa jengo la utawala hivyo kuona ulazima wa kuwepo kwa ulinzi madhubuti wa rasilimali za serikali, watumishi, wananchi na mali zao.

Mwakisu alisema kuwa eneo hilo kwa sasa limekuwa na shughuli za kiuchumi zimeongezeka baada ya kujengwa kwa jengo la utawala la halmashauri hivyo kuwepo kwa ongezeko kubwa la idadi ya watu na kwao kwa kuzingatia umuhimu wa kuwepo kwa hali ya Amani na usalama ndipo halmashauri imetoa fedha kwa ajili ya mradi huo.

Akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu Mhandisi wa ujenzi wa halmashauri ya wilaya Kasulu, Msakila Laurent alisema kuwa kiasi cha shilingi milioni 114.4 zimetumika kutekeleza mradi huo kutokana na umuhimu wa ulinzi na usalama katika eneo hilo…mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI