NA MATUKIO DAIMA MEDIA.
ZANZIBAR.Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuendelea na mpango wa kujenga masoko mapya ya kisasa katika maeneo ya Mwera, Kisauni, Fuoni na Kwa Haji Tumbo ili kuondoa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na kutoa mazingira bora ya kufanyia biashara.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika Soko la Mwanakwerekwe, Dk. Mwinyi alisema soko hilo tayari limekuwa dogo kutokana na wingi wa wafanyabiashara, hivyo kuna ulazima wa kupanua na kujenga masoko mengine ya kisasa.
“Tatizo la vibaraza litabaki historia tukiongeza masoko mapya. Niliahidi mitaji, na kwa kiwango kikubwa tumeweza kuwafikia. Tutaendelea kuongeza nguvu ili wafanyabiashara wote wapate maeneo mazuri ya kufanyia kazi zao kwa heshima na staha,” amesema Dk. Mwinyi.
Dk. Mwinyi pia amebainisha kuwa Serikali itaongeza fungu la mikopo na kuweka utaratibu nafuu wa kodi ya shilingi 30,000 ili wafanyabiashara waweze kuimudu bila mzigo mkubwa.
Amwongeza kuwa katika kipindi kilichopita, Serikali yake ilitoa shilingi bilioni 96 kwa ajili ya mikopo ya kuimarisha mitaji ya wafanyabiashara, na ahadi hiyo itaendelezwa kwa nguvu zaidi.
Aidha, amewataka wafanyabiashara hao kuhakikisha wanaiunga mkono CCM katika uchaguzi mkuu ujao ili kuendeleza kasi ya maendeleo.
“Kama mnataka uongozi unaoacha alama, basi tuendelee kushika madaraka. Tuliyoyaahidi mwaka 2020 tumetekeleza kwa vitendo, na mkinitia tena madarakani maendeleo yatakuja mara mbili zaidi. Nipigieni kura mimi kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar, Dk. Samia kwa Urais wa Jamhuri ya Muungano, pamoja na wagombea wetu wa Ubunge, Uwakilishi na Udiwani,” amesisitiza.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wa soko hilo kupitia mwenyekiti wao, Nyundo, walimhakikishia Dk. Mwinyi kuwa bado wana imani kubwa naye na watahakikisha kila mmoja anakuwa balozi wa mwenzake kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Wafanyabiashara hao walimueleza changamoto zao ikiwemo ukosefu wa mikopo licha ya uwepo wa benki 8 zilizojitokeza awali bila kutekeleza ahadi, mzigo mkubwa wa kodi kutokana na mfumuko wa bei, pamoja na ucheleweshaji wa mizigo bandarini ambao mara nyingi huwasababishia hasara.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohammed Said Mohammed, aliwahimiza wafanyabiashara hao kuendelea kumuunga mkono Dk. Mwinyi na wagombea wa CCM, akiwakumbusha kuwa mwaka 2020 aliahidi kujenga masoko ya kisasa na utekelezaji wake tayari unaonekana kwa vitendo.



.jpeg)






0 Comments