Header Ads Widget

ASKOFU MKUU NOVATUS RUGAMBWA AZIKWA BUKOBA, MAMIA WAMUAGA KWA HESHIMA.

 



Na Shemsa Mussa -Matukio Daima Media, Kagera.


WAUMINI wa Kanisa Katoliki na wananchi kutoka maeneo mbalimbali wamekusanyika katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma, Jimbo Katoliki la Bukoba, kushiriki misa ya mazishi ya Askofu Mkuu Novatus Rugambwa aliyefariki dunia Septemba 16, 2025 huko Roma.


Mazishi hayo yaliongozwa na viongozi Wa Kanisa Katoliki nchini, wakiongozwa na maaskofu na Mabadre kutoka Katika majimbo mbalimbali. 


Askofu Rugambwa alizaliwa Oktoba 8, mwaka 1957 katika Kijiji cha Mishenye, Kata ya Maruku, Wilaya ya Bukoba,na aliweza kufanya kazi ya utumishi wa miaka 39 katika upadre na miaka 15 akiwa katika nafasi ya Uaskofu, aliheshimika kwa unyenyekevu, bidii, na moyo wake wa kujitoa kwa ajili ya wengine.


Katika utume wake, alijikita katika kusaidia watoto na vijana wasio na uwezo kielimu kwa kuwatafutia ufadhili wa masomo katika fani mbalimbali, ndani na nje ya nchi. Aliona elimu kama njia ya ukombozi na maendeleo ya jamii, na alitumia nafasi yake kuhakikisha wengi wanapata fursa hiyo.


Mbali na elimu, Askofu Rugambwa alijitolea kusaidia mapadre na watawa kupata ufadhili wa masomo ya juu pamoja na fedha za kutekeleza miradi ya kijamii kama shule, hospitali, na nyumba za malezi. Alikuwa kiungo muhimu kati ya kanisa na wadau wa maendeleo wa kimataifa.


Mwaka 2010, Baba Mtakatifu Benedikto alimteua kuwa Askofu Mkuu na kumtuma kuhudumu katika nchi mbalimbali ikiwemo Brazil, Katika nafasi hiyo, alihubiri injili ya amani na upendo katika mataifa mbalimbali, akiheshimika kama balozi wa imani na mshikamano wa kimataifa.


Baadhi ya viongozi wa dini walimkumbuka kama kiongozi aliyetoa maisha yake kwa ajili ya wengine. Huku wakieleza kuwa Alikuwa kielelezo cha upendo, unyenyekevu na uaminifu kwa Mungu.


Askofu Mkuu Novatus Rugambwa ameagwa rasmi na kuzikwa katika Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Bukoba, huku sala zikiendelea kumwombea. Waumini waliongozwa kusema, “Raha ya milele umpe Ee Bwana, na mwanga wa milele umwangazie. Apumzike kwa amani.”


Mwisho.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI