Mahakama maalum nchini Sudan Kusini imesema kuwa ina mamlaka ya kuwafungulia mashtaka Makamu wa Rais aliyesimamishwa Riek Machar na washtakiwa wenzake saba, wanaoshtakiwa kwa mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu.
Mahakama ilitupilia mbali mapingamizi yote ya timu ya wanasheria wa Machar kuhusu mamlaka yake, uhalali wa kesi hiyo, na madai kwamba alikuwa na kinga dhidi ya kushtakiwa.
Kesi hiyo itaendelea Jumatano. Machar ametupilia mbali mashtaka yaliyoletwa dhidi yake wiki mbili zilizopita.
Wameibua hofu ya kurudi kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mashtaka hayo yanatokana na shambulio la mwezi Machi lililofanywa na wanamgambo wanaodaiwa kuwa na uhusiano na Machar, na kusababisha vifo vya wanajeshi 250 na jenerali mmoja.
Tangu wakati huo, amekuwa chini ya kizuizi cha nyumbani.
Timu ya mawakili ya Machar ilidai kuwa makosa hayo ya uhalifu yasihukumiwe na mahakama ya kitaifa bali mahakama ya mseto chini ya Umoja wa Afrika, kwa mujibu wa Mkataba wa Amani wa 2018 uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano kati ya vikosi vyake na wale watiifu kwa Rais Salva Kiir.






0 Comments