WATANZANIA 1,700,000 WANAKADIRIWA KUISHI NA VVU
Na Hamida Ramadhan, Dodoma
SERIKALI imetenga zaidi ya shilingi bilioni 277 kila mwaka kwa ajili ya kugharamia huduma mbalimbali za Virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI nchini, ikiwa ni hatua ya kupunguza utegemezi wa wafadhili wa kimataifa katika mapambano dhidi ya janga hilo.
Hayo yameelezwa leo, Jumatano, Agosti 6, 2025, na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dkt. Samwel Sumba, alipokuwa akizungumza katika Maonesho ya 32 ya Wakulima Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, baada ya kutembelea mabanda ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwemo banda la TACAIDS.
Dkt. Sumba amesema kuwa uwekezaji huo mkubwa wa Serikali unaonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha afua za VVU na UKIMWI kwa kutumia rasilimali za ndani. Hatua hiyo inalenga kudhibiti kwa ufanisi zaidi maambukizi mapya na kuboresha maisha ya watu wanaoishi na virusi hivyo.
Aidha, ameeleza kuwa kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Athari za UKIMWI ya mwaka 2022/2023, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu wanaoishi na VVU kati ya 1,540,000 hadi 1,700,000. Kiwango cha maambukizi kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi kimefikia asilimia 4.4, ambapo wanawake wanaongoza kwa asilimia 5.6 ikilinganishwa na wanaume wenye asilimia 3.0.
Hata hivyo, Dkt. Sumba ameongeza kuwa pamoja na takwimu hizo, bado kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha zaidi ya miaka ishirini iliyopita.
Maonesho ya Nanenane mwaka huu yameendelea kuwa jukwaa muhimu, si tu kwa sekta ya kilimo na mifugo, bali pia kwa taasisi mbalimbali za kijamii na kiafya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya msingi ya maendeleo ya binadamu, ikiwemo afya ya jamii.
0 Comments